2014-02-14 14:49:34

Majibu ya Papa Francisko kwa wanandoa watarajiwa!


Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani kwa Mwaka 2014 amewataka vijana kukuza na kujenga ndani mwao upendo unaodumu hadi kifo kitakapowatenganisha; wajitahidi kumwilisha ndani mwao mtindo wa maisha ya wanandoa ili kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia pamoja na kuthamini adhimisho la Sakramenti ya Ndoa ya Kikristo, kwani hapo wanajichotea neema na baraka katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema, upendo wa maisha ya ndoa ni wa kudumu hadi pale kifo kitakapowatenganisha kwani haya ni mahusiano kati ya Bwana na Bibi, yanayokuwa na kukomaa hatua kwa hatua, kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni upendo unaowashirikisha wanandoa kazi ya uumbaji na kamwe si upendo mpito usioguswa na mahangaiko ya mwenzi wake. Upendo huu hauna budi kurutubishwa kwa kukutana na Yesu kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na Matendo ya huruma.

Ubora wa ndoa unajikita katika udumifu wake, changamoto kubwa kwa wanandoa Wakristo. Pale wanandoa wanapohisi kwamba, wamepungukiwa na divai ya upendo na udumifu wasisite kumshirikisha Kristo katika upendo wao wa kila siku; ili wapendane na kutakiana mema.

Baba Mtakatifu anawaambia wanandoa watarajiwa kwamba, kuishi kwa pamoja ni sanaa na hija inayohitaji uvumilivu, inapendeza na kushangaza; ni safari inayojikita katika maneno: tafadhali, asante na samahani. Huu ni urithi ambao wanandoa wanapaswa kuwarithisha watoto wao. Ikumbukwe kwamba, unyenyekevu ni fadhila inaondoa chuki na kujenga upendo.

Si rahisi sana watu kujenga utamaduni wa kushuruku, lakini wanandoa wajenga na kuimarisha utamaduni wa kushuruku kwani mwenzi wako ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha. Wanandoa wajifunze kutambua mapungufu yao ya kibinadamu na kuwa tayari kukiri makosa yao, tayari kuanza tena upya. Wajenge utamaduni wa kusikilizana kwa makini, ili kujenga na kuimarisha familia ya Kikristo.

Baba Mtakatifu anasema hakuna Familia inayoweza kujidai kwamba ni kamilifu na takatifu; wala hakuna Bwana au Bibi ambaye ni mkamilifu, kila mtu ana fadhila na kasoro na mapungufu yake, changamoto ya kujenga utamaduni wa kuomba na kutoa msamaha kila siku na kwa njia hii Ndoa zinaweza kudumu daima.

Maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa Kanisani yazingatie umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa na kiasi bila kumezwa mno na malimwengu. Watambue uwepo wa Yesu Kristo anayeendelea kufanya miujiza kwa wanandoa kama alivyofanya takribani miaka elfu mbili iliyopita kwenye Arusi ya Kana. Kila kitu kiwe na kiasi na kielelezo cha furaha ya ndani na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanandoa wawashirikishe jirani zao ile furaha na kumbu kumbu ya maisha yao ya ndoa.

Haya ndiyo yaliyojiri katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao Duniani kwa Mwaka 2014, tukio ambalo litakumbukwa na wanandoa hawa watarajiwa katika hija ya maisha yao ya ndoa na familia. Mji wa Roma, umefurika umati wa vijana na wasichana wanaotembea huku wameshikana mikono na maua ya waridi mikononi mwao alama ya upendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.