2014-02-14 10:07:58

Kongamano la Kimataifa kuhusu Waraka wa Liturujia ya Kanisa


Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kuanzia tarehe 18 hadi 20 Februari 2014 litaadhimisha Kongamano la Kimataifa, kuhusu Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Liturujia ya Kanisa "Sacrosanctum Concilium", litakaloongozwa na kauli mbiu Waraka wa Liturujia, shukrani na dhamana kwa ajili ya mabadiliko ya Kikanisa".

Kongamano hili litawashirikisha wadau kutoka sehemu mbali mbali za dunia na utakuwa ni muda muafaka kwa ajili ya kusali, kutafakari, kuabudu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Ni kipindi cha kuonjeshana uzoefu na mang'amuzi ya Liturujia ya Kanisa, tayari kutweka hadi kilindini kwa ajili ya kuendeleza dhamana ya Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa.

Akizungumzia kuhusu Kongamano hili la Kimataifa litakalofanyika kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano, Askofu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema mabadiliko ya Liturujia ya Kanisa ni sehemu ya mchakato mzima wa mageuzi yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuhimiza mambo yale yanayoleta umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo; kwa kujali, kurekebisha na kukuza Liturujia inayodhihirisha Fumbo la maisha ya Kristo na maumbile halisi ya Kanisa, kwa kuwajenga na kuwaimarisha waamini katika mchakato wa kuelekea katika ukamilifu.

Ni kwa njia ya Liturujia Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa na kwamba, Kristo hushiriki daima katika Kanisa lake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa milele. Kanisa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wake, kwa kuwataka waamini kufanya rejea mara kwa mara katika mafundisho yanayotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya maisha yao kiroho.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Mama Kanisa ni kutaka kuhakikisha kwamba, waamini wanafundwa kikamilifu kuhusiana na Liturujia ya Kanisa ili waweze kuwa na ushiriki mkamilifu bila kusahau kuwaandaa wataalam katika Liturujia, ili kuendeleza mchakato wa mabadiliko yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Tafsiri ya vitabu vya Liturujia katika lugha mbali mbali pamoja na mchakato wa utamadunisho ni kati ya matunda makuu yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Liturujia kiwe ni kipindi cha kufanya upembuzi yakinifu kuhusu Fumbo la Kanisa linalosali na kuhamasishwa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Ushuhuda huu unabubujika kutoka katika Kanisa linalosali na kuinjilisha.

Kwa upande wake KardinaliAntonio Canizares Llovera, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema, Waraka wa Liturujia ni kielelezo cha Pentekoste mpya ndani ya Kanisa iliyoleta mwanga wa matumaini mapya katika mchakato wa mabadiliko ya ndani, kwa kukazia mshikamano wa upendo unaobubujika kutoka ndani ya Kristo na Kanisa lake kwa ajili ya binadamu wote.

Kanisa likajikuta linaanza mchakato wa mageuzi na kujitakasa, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, changamoto ya kuendeleza dhamana hii katika ulimwengu wa utandawazi. Waamini wajitaabishe kusoma nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa ajili ya kushiriki katika maboresho ya maisha na utume wa Kanisa. Liturujia ya Kanisa iwawezeshe waamini kulifahamu, kuliadhimisha na kushiriki kikamilifu Fumbo la Maisha ya Kristo.

Liturujia ni chemchemi ya maisha ya kimungu, shule ya kwanza ya moyo wa mwanadamu na zawadi ya kwanza inayowaunganisha waamini katika imani na maisha ya sala, changamoto ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Katika Liturujia Fumbo la Utatu Mtakatifu linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; waamini wajitengee muda wa kutafakari Neno la Mungu,

Kongamano la Kimataifa kuhusu Liturujia linaongozwa na maneno makuu mawili: kushukuru na dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi kwa sasa ili kuhakikisha kwamba, mabadiliko yaliyoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kujikita katika Uinjilishaji Mpya kwa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani; ili kujenga na kukuza ari na moyo wa watu wa Mungu waliotakaswa tayari kujitosa kimasomaso kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na upendo.

Akichangia mada kuhusu Kongamano hili la Kimataifa, Askofu Enrico Covolo, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano anasema, Kanisa linayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mang'amuzi na busara iliyooneshwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa.

Kati ya matunda ya mabadiliko haya ni umoja na mshikamano wa Kikanisa; umuhimu wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu lenye mwelekeo wa Kijumuiya na Kikanisa na kutambua kwamba, waamini wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Liturujia inakuwa ni shule ya Sala za Kikristo na chachu ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.