2014-02-14 14:57:45

Epukeni kishawishi cha kugeuka na kuwa ni Mbwa mwitu badala ya Kondoo!


Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu, kumbu kumbu ya Watakatifu Cyril na Metodi, iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 14 Februari 2014 amewakumbusha waamini kwamba, wanatumwa kama Kondoo kati ya Mbwa mwitu na kamwe wasigeuke na kuanza wao wenyewe kuwa ni Mbwa mwitu, kinyume cha agizo la Kristo. Injili ya Kristo inatangazwa kwa furaha na wala litania ya malalamiko haina nafasi.

Wakristo wanakumbushwa kwamba, wameitwa na kutumwa na Kristo kutangaza Injili ya Furaha kila pembe ya dunia wakitambua kwamba, njiani watakumbana na "majanga" ya maisha, lakini hawana sababu ya kuogopa, lakini bado waendelee kutunza utambulisho wao wa Kikristo. Kamwe waitumbukie katika kishawishi cha kugeuka na kuwa Mbwa mwitu, kwani Kristo anaweza kuwatema na kuwaacha soremba!

Furaha ni sehemu ya utambulisho wa maisha ya Mkristo, kwani ni kielelezo kwamba wamekutana na kuonana na Yesu, ambaye ni sababu ya furaha ya maisha yao. Katika shida na mahangaiko yao, Yesu yuko pamoja nao na yuko tayari kuwasaidia, kumbe Injili ya Kristo haina budi kusonga mbele kwa kushuhudiwa kwa njia ya furaha; huzuni na masikitiko yanachafua utambulisho huu wa Wakristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.