Wayahudi na Wakatoliki wanaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani
na maendeleo ya wengi!
Kamati ya Wayahudi kutoka Marekani imekuwa na uhusiano mzuri na Vatican na kwamba,
imechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi
na Wakatoliki, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican yapata
miaka hamsini iliyopita. Wayahudi na Wakatoliki wanao urithi mkubwa katika maisha
ya kiroho, msingi katika majadiliano ya kidini baina ya pande hizi mbili, kwa kutambua
kwamba, uhusiano wa pekee walionao mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hayo yamesemwa
na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 13 Februari 2014 alipokutana na kuzungumza
na wajumbe wa Kamati ya Wayahudi kutoka Marekani waliomtembelea mjini Vatican. Anasema,
Wayahudi na Wakatoliki wanaweza kushirikiana kwa pamoja katika kukoleza mchakato wa
ujenzi wa misingi ya haki, amani na udugu duniani; kwa kujikita katika huduma makini
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama yanavyohimiza Maandiko
Matakatifu. Huu ni utashi na haki ya Mungu dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini
wote.
Ili majadiliano ya kidini yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kuna haja
kwa wahusika kurithisha mang'amuzi ya urafiki, heshima na kuthaminiana ambayo yamefanyiwa
kazi katika kipindi cha miaka yote na Tume ya Wayahudi kutoka Marekani. Ni matumaini
ya Baba Mtakatifu kwamba, Tume hii itaendeleza tema juu ya uhusiano kati ya Wayahudi
na Wakatoliki katika: Seminari na vituo mbali mbali vya elimu kwa waamini walei ndani
ya Kanisa Katoliki sambamba na Marabbi nao kujitahidi kufahamu Ukristo.
Baba
Mtakatifu amewaambia kwamba, baada ya muda si mrefu anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji
katika Nchi Takatifu, anawaalika na kuwaomba, ili waweze kumsindikiza katika sala
zao ili hija hii ya maisha ya kiroho iweze kuzaa matunda ya umoja, matumaini na amani.