Usipokuwa makini, imani yako inaweza kuzimika kama kibatari!
Mwamini anaweza kupoteza dira na mwelekeo wa imani yake kwa kukumbatia malimwengu
na kwa upande mwingine mtu asiyeamini katika unyenyekevu wake anaweza kukirimiwa zawadi
ya imani na kuwa ni mfano na kielelezo cha kuigwa kama ilivyojitokeza kwa Mwanamke
Myunani aliyempigia Yesu magoti akitaka huruma na upendo kwa ajili ya mtoto wake aliyekuwa
anasumbuliwa na pepo mchafu.
Baada ya majadiliano ya kina, Yesu anamponya
mtoto wake kutokana na imani kubwa aliyoonesha Mama yule mbele ya Yesu.
Ni
maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican siku ya Alhamisi, tarehe
13 Februari 2014. Anasema, kuna kundi kubwa la waamini ndani ya Kanisa linalofanya
hija ya kutaka kukutana na Yesu katika maisha yao, kwa kusukumwa na Roho Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu anaonya kwamba, kuna baadhi ya watu wamelewa mno madaraka pamoja na kumezwa
na malimwengu, kiasi cha kuthubutu kuharibu uhusiano mwema waliokuwa nao mbele ya
Mwenyezi Mungu, kwa kukumbatia ukahaba uliowasaliti, kama ilivyotokea kwa Mfalme Sulemani,
aliyekuwa na hekima, busara na nguvu nyingi, lakini mbele ya wanawake "akanywea na
kuzimika kama kibatari kiasi cha kupoteza imani yake! Inaweza pia kutokea kwa waamini
kuifahamu Kanuni ya Imani kwa kichwa lakini wakajikuta kwamba, hawana tena imani.
Mfalme
Sulemani alikuwa mdhambi kama baba yake Daudi, lakini akaelemewa na udhaifu wake kiasi
kwamba, akajikuta anakuwa ni fisadi na jeuri kiasi cha kushindwa kuomba msamaha kama
alivyofanya Mfalme Daudi na matokeo yake akapoteza imani kutoka katika undani wa moyo
wake.
Neno la Mungu linapaswa kupokelewa na kumwilishwa katika maisha ya unyenyekevu
kama alivyofanya yule mwanamke Myunani anayesimuliwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu,
kiasi hata cha kukirimiwa ukombozi.