Yafuatayo ni maelezo ya Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ya Tanzania katika mkutano wa Tanzania Centre for democracy, kuhusu tafakuri
na maridhiano kuelekea Katiba mpya ya Tanzania, mkutano uliofanyika Jijini Dar es
Salaam, tarehe 12 februari 2014
1.0 UTANGULIZI Katika nchi yoyote, msingi
wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba ambayo ni sheria kuu. Sheria zote hutungwa
kwa kuzingatia masharti ya Katiba. Katiba huainisha misingi ya Taifa, mgawanyo wa
madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, usimamizi wake, mgawanyo na ukomo
wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola. Kwa ujumla Katiba ni makubaliano ya wananchi
husika kuhusu utaratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao.
Kutokana
na maana hiyo ya Katiba, utungaji wake unatakiwa kuwa shirikishi kwa maana ya kuwahusisha
wananchi katika hatua zote za mchakato wa kupata Katiba. Kadri mchakato wa kuandika
Katiba unavyowashirikisha wananchi kwa mapana, ndivyo kukubalika, kuheshimika na utekelezaji
wa Katiba utakavyokuwa rahisi. Wananchi wanaposhiriki katika utungaji wa Katiba, na
pale matakwa yao yanapozingatiwa ndani ya Katiba, Wananchi hao huimiliki Katiba hiyo
na kuiona kuwa ni Katiba yao. Wananchi huona hivyo kwa sababu licha ya kushiriki lakini
pia katiba hiyo huakisi utashi wao na ndoto zao na hivyo kukubali kuongozwa na masharti
yaliyomo ndani ya Katiba.
Mchakato wa katiba kwa kadri unavyowashirikisha wananchi,
ndivyo unavyowezesha kupatikana kwa mwafaka wa kitaifa kuhusu misingi, malengo na
namna serikali na vyombo vyake vitakavyoongoza nchi. Mwafaka huo huzaa katiba ya wananchi
ambayo inaimarisha umoja, udugu, ushirikiano na mshikamano katika Taifa kwa maendeleo
na ustawi wa jamii.
1.1 Maana na sababu za Mchakato wa Katiba Mchakato
wa Katiba hulenga kupata Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo. Michakato
mingi ya Katiba hujumuisha Kanuni na hatua kama ifuatavyo: (a) kukubaliana
kuhusu mambo yote yanayohitajika na kupanga malengo; (b) kukubaliana kuhusu
vyombo vya Kusimamia na utaratibu utakaotumika; (c) kuandaa Wananchi kwa kutoa
elimu ya Katiba; (d) kukusanya Maoni ya Wananchi wa aina zote; (e) kushauriana
na Wataalam; (f) kujifunza kutokana na Uzoefu wa Nchi mbalimbali; (g)
kuchambua na kutathmini maoni ya Wananchi; (h) kuandika Toleo la Kwanza la Rasimu
ya Katiba; (i) Wananchi Kujadili Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba; (j)
Kuchambua na kutathmini maoni ya wananchi kuhusu Toleo la Kwanza la Rasimu ya Katiba; (k)
Bunge Maalum kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba; (l) Wananchi kuridhia
Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalum kupitia Kura ya Maoni; (m) kuzindua kutumika
kwa Katiba Mpya; (n) utekelezaji wa Katiba Mpya. Utekelezaji wa Masuala
na hatua zote zilioainishwa hapo juu ndio unatafsiriwa kuwa “Mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba.” Katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea katika nchi
yetu, Kanuni na hatua hizi zimeainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura
ya 83.
Msingi wa kuwa na mchakato wa katiba ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki
katika hatua zote za kupata Katiba na hivyo kuijengea uhalali.
2.0 UTARATIBU
WA KUFANYA MABADILIKO YA KATIBA Katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba, zipo njia
kadhaa ambazo hutumika. Njia hizo ni: (a) Rais kuanzisha mchakato wa mabadiliko
ya katiba; (b) kuunda Tume ya kuandaa Katiba kupitia sheria zilizopo; au (c)
Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko ya katiba.
2.1 Rais kuanzisha
mchakato wa mabadiliko ya katiba Kama ilivyoelezwa hapo juu, mojawapo ya njia za
kufanya mabadiliko ya Katiba ni kwa Rais kuanzisha mchakato huo. Katika utaratibu
huu, Rais huagiza wataalamu wa kuandika katiba kutayarisha Rasimu ya Katiba. Mara
baada ya Rasimu kutayarishwa, Rais humuagiza Waziri kuwasilisha Rasimu hiyo katika
chombo cha uwakilishi. Chombo cha uwakilishi hupewa muda maalum wa kujadili na kupitisha
Rasimu hiyo bila kujali kuwa maudhui ya Rasimu husika yanaakisi maoni au matakwa ya
wananchi. Kimsingi, katiba inayopatikana kwa utaratibu huu hutokana na utashi na matakwa
ya Rais au Serikali iliyopo madarakani. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na aliyekuwa
Rais wa Misri Bw. Morsi na pia unaendelea kutumiwa na Utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
2.2 Kuunda Tume ya kuandaa Katiba kupitia sheria zilizopo Utaratibu
mwingine wa mchakato wa mabadiliko ya katiba hufanywa kupitia Tume inayoundwa kwa
mujibu wa sheria zilizopo ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali
katika Nchi. Chini ya utaratibu huu, Rais au Waziri mwenye dhamana ya masuala ya katiba,
kwa mamlaka anayopewa na sheria husika huunda Tume au Kamati za kushughulikia mchakato
wa mabadiliko ya katiba.
Tume au Kamati inayoundwa hupatiwa hadidu za rejea
na muda maalum wa kukamilisha mchakato. Ripoti ambayo itaandikwa kutokana na mchakato
uliofanyika, hutumiwa na Serikali kuandaa Rasimu ya Katiba au sheria ya marekebisho
ya Katiba. Hata hivyo, licha ya mchakato huu kutowashirikisha wananchi kwa upana na
uwazi, Serikali hailazimiki kufanya mabadiliko yoyote ya katiba na inaweza kukalia
Ripoti na kupuuza matakwa ya wananchi.
Aidha, mchakato wa mabadiliko unaofanywa
na Tume au Kamati kupitia utaratibu huu huzingatia hadidu za rejea zilizotolewa na
Serikali, ambazo wakati mwingine haziakisi, matakwa au madai ya wananchi. Ghana, Uganda
Zimbabwe na Zambia ni miongoni mwa nchi zilizowahi kufanya au kujaribu kufanya mabadiliko
ya Katiba kwa kutumia utaratibu huu.
2.3 Bunge kutunga sheria maalum ya mabadiliko
ya katiba Utaratibu mwingine wa mchakato wa mabadiliko ya katiba ni wa kutunga
sheria mahsusi ya kushughulikia mabadiliko ya katiba. Katika utaratibu huu, sheria
inayotungwa hueleza utaratibu wa mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Utaratibu
huu ni shirikishi kwani wananchi hushirikishwa kisheria katika hatua zote muhimu za
uandikaji wa katiba yao. Chini ya utaratibu huu, hadidu za rejea hutolewa na sheria
yenyewe badala ya Rais au Waziri. Aidha, Tume hupewa jukumu la kuratibu, kukusanya
maoni ya wananchi, kuyachambua na kutathmini maoni kabla ya kuandaa ripoti na Rasimu
ya Katiba. Mara baada ya kuandaa Rasimu ya Katiba, wananchi hupewa tena fursa ya kutoa
maoni yao kabla ya Tume au Kamati kuifanyia marekebisho na kuiwasilisha katika Baraza
au Bunge Maalum la Katiba.
Baraza au Bunge Maalum huwa na jukumu la msingi
la kuijadili na kuipitisha Rasimu ya Katiba. Katika baadhi ya nchi kama vile Afrika
Kusini, Ghana na Uganda, mchakato wa Katiba Mpya ulikamilishwa na Bunge Maalum. Baadhi
ya nchi pia hazikutumia Bunge Maalum na badala yake, Rasimu ya Katiba ilipigiwa kura
ya “Ndio” au “Hapana” baada ya kutoka kwenye Tume au Kamati. Kwetu Tanzania, Sheria
inayosimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba imeainisha hatua zote tatu ambazo ni
Tume kuandaa Rasimu ya Katiba, Bunge Maalum kujadili Rasimu ya Katiba na kupitisha
Katiba ambayo itapendekezwa kwa wananchi ili kuipigia kura ya maoni.
3.0
MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA Mwaka 2011, Taifa la Tanzania lilianzisha
mchakato wa mabadiliko ya katiba. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania,
Bunge lilitunga sheria mahsusi ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba. Sheria
hiyo inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imeweka masharti kuhusu
usimamizi na uendeshaji wa mchakato wa mabadiliko ya katiba. Sheria hii imempatia
mamlaka Rais kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kushauriana na kukubaliana
na Rais wa Zanzibar.
Katika kutekeleza matakwa hayo, Sheria ilimtaka Rais
kualika Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, Jumuiya za Kidini, Asasi za Kiraia,
Jumuiya na Taasisi zisizo za Kiserikali na Makundi ya Watu wenye Malengo Yanayofanana
kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume .
Sheria
hiyo imeainisha utaratibu wa utendaji kazi wa Tume na Hadidu za Rejea ambazo ni: (a)
kuratibu na kukusanya maoni ya Wananchi; (b) kupitia na kutafiti usahihi na
ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya wananchi, mifumo ya kisiasa,
demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora; (c) kutoa mapendekezo kwa kila
Hadidu ya Rejea; na (d) kuandaa na kuwasilisha Ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi. Sheria hiyo pia, inaainisha Misingi ya Kitaifa na Maadili ambayo
yanapaswa kuzingatiwa na Tume katika mchakato wa kupatikana Katiba Mpya. Misingi hiyo
ni: (a) kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano; (b) uwepo wa Serikali, Bunge na
Mahakama; (c) mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) uwepo wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar;
(e) umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(f)
uchaguzi wa kidemokrasia na wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia
haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
(g) ukuzaji na uhifadhi wa
Haki za Binadamu;
(h) utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria;
na
(i) uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu
uhuru wa kuabudu.
Kwa ujumla, Sheria inaainisha kazi na majukumu ya Tume kuwa
ni: (a) kuandaa na kuendesha programu za elimu kwa umma juu ya madhumuni na
majukumu ya Tume; (b) kuitisha na kusimamia mikutano au Mabaraza ya Katiba katika
sehemu na nyakati mbalimbali kama itakavyoamua; (c) kutathmini na kuchambua
maoni ya wananchi yanayokubaliana na yale yasiyokubaliana; na (d) kutayarisha
na kuwasilisha Ripoti kwa kuzingatia Hadidu za Rejea. Katika kutekeleza kazi na
majukumu yake, Tume imepewa mamlaka ya: (a) kumtaka mtu yeyote, atakayehiari,
kwenda mbele yake na kufanya naye majadiliano kwa mazungumzo au kuwasilisha nyaraka; (b)
kupitia na kufanya uchambuzi wa michango, mawazo, maoni, taarifa na mapendekezo yaliyotolewa
na kufanyiwa tathmini siku za nyuma, kupitia nyaraka mbalimbali zilizoainishwa katika
Sheria hiyo, na nyingine zozote ambazo Tume itaona zinafaa; (c) kumtaka Mkuu
wa Wilaya, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Afisa Mtendaji wa Kata au Afisa
Mtendaji wa Kijiji kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji, Kata, Mtaa au Kijiji kwa Tanzania
Bara; (d) kumtaka Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, Katibu wa Halmashauri
ya Mji au Wilaya, au Sheha kuitisha mkutano wa Wakazi wa Mji au Shehia, kwa upande
wa Zanzibar; (e) kuunda Kamati kwa ajili ya kazi za jumla au maalum; (f)
kumtumia au kumshirikisha mtaalamu mwelekezi au mtu yeyote kadri itakavyokuwa lazima;
na (g) isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, kutumia utaratibu unaofanana
wa ukusanyaji na uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba
na uandaaji wa Ripoti.
Sheria pia imeainisha kuwepo kwa Bunge Maalum la Katiba
na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, utaratibu wa kuwapata Viongozi na Sekretarieti
ya Bunge Maalum la Katiba umeainishwa katika Sheria hii. Sheria pia imeainisha utaratibu
wa Bunge Maalum kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na Utaratibu
wa Majadiliano ya kupitisha Rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kwa Wananchi ili kuipigia
kura ya maoni.
Katiba itapitishwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wajumbe
kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wajumbe kutoka Zanzibar. Utaratibu wa kura
ya maoni na Uzinduzi wa Katiba mpya pia umeainishwa.
Kwa kifupi, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni Katiba au Msahafu wa Mchakato wa Mabadiliko ya
Katiba unaoendelea hivi sasa. Sheria imeunda vyombo vyote muhimu na kila chombo kimepewa
hadidu za rejea. Kila chombo kimewekewa utaratibu wa kazi na madaraka yake. Katika
utaratibu huu kila chombo kina madaraka yake yaliyowekewa mipaka. Haiyamkini kwa Tume
kukusanya maoni, kuandika Rasimu ya Katiba, kuiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba
kisha nayo ishiriki kuijadili Rasimu ya Katiba. Au, Bunge Maalum la Katiba, lenye
madaraka ya kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba wakati huo huo kuandika Rasimu
ya Katiba mbadala au kubadili mfumo wa Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Hivyo
hivyo, kwa Tume ya Uchaguzi na Wananchi. Kila aliyetajwa, ikiwa ni pamoja na Rais
wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, ana jukumu maalum lililoainishwa na Sheria.
4.0
WAPI TULIPO HIVI SASA
Kufuatia Tume kukabidhi Ripoti na viambatanisho vyake
kwa Marais, kama Sheria inavyoelekeza Rais amekwishachapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine vya habari, amekwishateua
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na kuliitisha Bunge Maalum la Katiba ili kukutana
kuanzia tarehe 18 Februari, 2014, Dodoma. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba atawasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge
Maalum. Bunge hilo litakuwa na wajibu wa kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba kabla
ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
5.0 BUNGE MAALUM NA MAJUKUMU YAKE
Bunge
Maalum la Katiba ni chombo cha uwakilishi kama lilivyo Bunge la kawaida isipokuwa
Bunge Maalum la Katiba huundwa kwa ajili tu ya kutunga Katiba na kufanya shughuli
zingine zinazoambata na utungaji wa Katiba. Bunge Maalum la Katiba hupewa jukumu hili
la kutunga katiba badala ya Bunge la kawaida kwa sababu Bunge Maalum la Katiba linawakilisha
wananchi ambao ndio msingi wa mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote ikiwemo Bunge
la kawaida ambalo pia ni zao la Katiba.
Majukumu ya Bunge la Maalum la Katiba
yanaweza kutofautina kulingana na namna utaratibu mzima wa mchakato wa mabadiliko
ya katiba ulivyopangwa. Katika baadhi ya nchi, Bunge Maalum la Katiba hupewa mamlaka
ya kusimamia mchakato wote wa mabadiliko ya katiba, wakati katika nchi nyingine Bunge
hili hushirikiana na vyombo vingine katika kufanya na kusimamia mchakato wa mabadiliko
ya katiba.
5.1 Madaraka ya Bunge Maalum Madaraka ya Bunge Maalum yamekuwa
yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika. Afrika kusini, Namibia na
Cambodia Bunge Maalum lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika Rasimu ya Katiba.
Katika mazingira haya, Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi
katika Rasimu ya Katiba. Bunge Maalum lilikuwa na madaraka ya kuachana na Rasimu ya
Katiba na kuandika Rasimu Mbadala.
Madaraka ya Bunge Maalum yanakuwa na mipaka
endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko ya Katiba au Chombo cha aina
hiyo. Bunge Maalum linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye
Rasimu ya Katiba lakini si suala la kawaida Bunge Maalum kubadili hoja ya msingi.
Jinsi ushirikishaji wa Wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge
Maalum yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia Bunge Maalum kunyang’anya madaraka ya Wananchi,
yaani “act of popular sovereignty”. Wataalam wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa
madaraka ya Bunge Maalum katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge
Maalum limepewa madaraka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba, kutunga Sheria
ya Masharti ya Mpito na Masharti yatokanayo na kabla ya kuanza kazi hiyo, Bunge Maalum
litapitisha Kanuni za Bunge Maalum ambazo zitaongoza utekelezaji wa mamlaka ya Bunge
Maalum.
5.2 Kanuni za Bunge Maalum Kanuni za Bunge Maalum la Katiba sharti
zizingatie kwamba Bunge Maalum, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini ya kifungu
cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ni chombo cha kuboresha
masharti ya Rasimu ya Katiba.
Katika kutekeleza madaraka ya kujadili na kupitisha
masharti ya kikatiba, Bunge Maalum litazingatia msingi kwamba masharti ya kikatiba
ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto za Wananchi ambazo zimeelezwa
kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya wananchi kupitia asasi, taasisi,
jumuiya na makundi ya Watu Wenye Malengo Yanayofanana. Bunge Maalum litafanya
kazi ya kuboresha masharti ya Kikatiba yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo kuweka
masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha masharti ya kikatiba
yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
6.0 MUUNDO WA MUUNGANO WA SERIKALI TATU
Muundo
wa Muungano umewekwa katika Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Ili kupata maana kamili
ya muundo wa Muungano unaopendekezwa, Tume ni vema kusoma Sura ya Kwanza, Sura ya
Nane na Sura ya Kumi na tano. Taswira ya Muungano wa Serikali Tatu unaopendekezwa
katika Rasimu ya Katiba imejengwa katika Ibara ya 1 inayoieleza Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuwa ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili – Sovereign Federal Republic.
Kwa hali hiyo Muungano wa Serikali Tatu haubadili hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika
jumuiya ya kimataifa kuwa ni nchi moja. Kupendekezwa kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika
haina maana ya kuunda nchi mpya. Kinachopendekezwa ni kutenganisha mamlaka ya Mambo
ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Tanganyika na Zanzibar hazina
hadhi ya Jamhuri, na kwa hiyo si “Sovereign States” kama ilivyo Jamhuri ya Muungano.
6.1 Misingi ya Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu Muungano wa Serikali
Tatu unaopendekezwa umezingatia mamlaka tatu zilizomo ndani ya Jamhuri ya Muungano
hivi sasa: (a) Mamlaka ya Mambo ya Muungano –Jurisdiction on Union Matters
yanayosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4(2), (3)
na 34(1) na (3) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977;
(b)
Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Zanzibar yanayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa kupitia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa Ibara ya
4(2) na (3), 64(2) na (5) na Ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977; na (c) Mamlaka ya Mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika ambayo
kwa sasa yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa - Ibara
ya 4, 34(2) na (3) na 64 (4). Kila mamlaka sasa itakuwa na Serikali yake ambayo
itasimamiwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
6.2 Mgawanyo wa majukumu
na madaraka katika Serikali tatu Ibara ya 60 na Nyongeza ya Kwanza inaorodhesha
mambo saba ya Muungano ambayo yanasimamiwa na Jamhuri ya Muungano. Haya ndiyo masuala
makuu na ya msingi ya kidola (Sovereign Functions) ambayo ndiyo yalivyo katika masuala
11 ya Muungano yaliyomo katika Hati ya Muungano ya Mwaka 1964.
Katika mambo
haya saba, Jamhuri ya Muungano inayo mamlaka kamili tena yasiyogawanyika. Mambo hayo
7 hayawezi kufanywa na Serikali za Nchi Washirika wa Muungano kwa sababu hazina sifa
ya “Sovereign States”. Kwa mfano suala la ulinzi na usalama lipo moja kwa moja katika
Jamhuri ya Muungano. Pamoja na orodha ya mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika
Nyongeza ya Kwanza, zipo taasisi ambazo zimetajwa katika Rasimu ya Katiba kuwa za
Muungano lakini hazijaorodheshwa. Taasisi hizo na mambo hayo yamejumuishwa katika
Mambo ya Muungano Yaliyokusudiwa katika aya ya 1 ya Mambo ya Muungano, yaani – Katiba
na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
6.3 Hadhi ya Marais wanaotajwa
katika Rasimu ya Katiba Katika Rasimu ya Katiba yumo Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar. Ingawa wote wanaitwa Rais, lakini
hawafanani kwa hadhi na majukumu. Rais mwenye mamlaka juu ya Jamhuri ya Muungano ni
Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri
ya Muungano ndiye peke yake Mkuu wa Nchi mwenye mamlaka kamili (Head of State), Amiri
Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali ya Muungano. Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar
hawana sifa hizo ingawa wao ni wakuu wa mambo yote yasiyo ya Muungano katika maeneo
yao ya utawala. Kwa kuhakikisha hilo, Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar hawakupewa
hadhi ya Makamu wa Rais kwa makusudi. Kwa msingi huo hawawezi kukaimu nafasi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano akisafiri au akiwa hawezi kutekeleza kazi kwa muda. Hilo likitokea
wanaweza kukaimu ni Makamu wa Rais, Waziri Mwandamizi, n.k.
6.4 Misingi ya
utendaji ya Muungano wa Serikali Tatu Muundo wa Serikali Tatu umejengwa katika
Misingi ya Utendaji (Principles) ifuatayo: (a) Muungano wa Hiari (Voluntary
Union); (b) ushirikiano ( Co-operation); (c) uratibu (Co-ordination); (d)
Mshikamano (Solidarity); na (e) subsidiarity.
6.4.1 Muungano
wa Hiari (Voluntary Union) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Muungano wa iliyokuwa
Jamhuri ya Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Msingi wa Muungano
huu ni Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964 yaliyofikiwa baina
ya mataifa haya mawili. Chini ya makubaliano hayo, mataifa hayo yalikubaliana kwa
hiari kuachia baadhi ya mamlaka na kuyapeleka mamlaka hayo katika Serikali ya Muungano.
Uhiari huu wa kukubali kuungana kwa mataifa haya mawili ni moja ya misingi ya utekelezaji
wa muundo wa Muungano unaopendekezwa wa Serikali Tatu. Ibara ya 1(3) ya Rasimu ya
Katiba inapendekeza pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano iwe ni msingi mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.4.2 Ushirikiano (Co-operation) Msingi
mwingine wa utendaji katika muundo wa Serikali Tatu ni Ushirikiano. Chini ya msingi
huu, Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika zitakuwa na ushirikiano baina
yao katika shughuli zote za utendaji na uendeshaji wa nchi ili mradi ushirikiano huo
haukiuki Katiba. Ibara ya 65(1) inapendekeza kuwa Nchi Mshirika iweze kuomba ushirikiano
kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha uhusiano wake wa kikanda
au kimataifa. Aidha, Ibara ya 66 inapendekeza masharti kuhusu ushirikiano kati ya
Nchi Washirika zenyewe na baina ya Nchi hizo na Serikali ya Muungano kwa lengo la
kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na kukuza maendeleo ya wananchi.
6.4.3
Uratibu (Coordination) Katika mfumo wa Serikali Tatu, uratibu wa uhusiano baina
ya Serikali hizo ni moja ya misingi muhimu. Ibara ya 67 inapendekeza kuwepo kwa Waziri
Mkaazi atakayeteuliwa na kila Nchi Mshirika atakayefanya kazi akiwa Makao Makuu ya
Serikali ya Muungano. Moja ya majukumu ya msingi ya Waziri Mkaazi ni kuratibu uhusiano
baina ya Serikali yake na Serikali nyingine ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake
na Serikali ya Muungano. Aidha, Ibara ya 109 inapendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Uhusiano
na Uratibu wa Serikali chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais. Kuwepo kwa uratibu kutaimarisha
uhusiano wa kiutendaji baina ya Serikali zinazopendekezwa na hivyo kuimarisha Muungano.
6.4.4
Mshikamano (Solidarity) Mshikamano (Solidarity) ni moja ya misingi muhimu ya utendaji
katika mfumo wa Shirikisho. Msingi huu umezingatiwa katika Rasimu inayopendekezwa
ili kuhakikisha kuwa Serikali zote tatu zinashikamana na kusaidiana katika kila hali
inayoweza kujitokeza. Mathalani, Ibara ya 62(3) inapendekeza kuipa Serikali ya Muungano,
kwa makubalino na masharti maalum na Serikali ya Nchi Mshirika, madaraka ya kutekeleza
jambo lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Nchi Mshirika. Aidha, Ibara ya
65 na 66 zinapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya Serikali za Nchi washirika
na kati ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Msingi huu ni muhimu katika kuhakikisha
kuwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika kwa usawa na mshikamano
baina ya Nchi Washirika.
6.4.5 Subsidiarity Msingi wa subsidiarity
unakusudia kuweka utaratibu wa mamlaka za chini kutekeleza majukumu yaliyo ndani ya
uwezo wake ikiwa mamlaka hizo zina uwezo wa kutekeleza majukumu hayo kwa ukamilifu.
Msingi huu wa subsidiarity unaruhusu mamlaka ya juu kutekeleza jambo ambalo kwa kawaida
hutekelezwa na mamlaka ya chini iwapo mamlaka ya juu ina uwezo wa kutekeleza jambo
husika kwa ufanisi au vinginevyo. Ibara ya 65 na 66 zimeweka msingi kwamba, ingawa
Serikali ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kushughulikia Mambo ya Muungano, Serikali
hiyo, kwa ridhaa ya Serikali ya Nchi Mshirika, itakuwa na mamlaka ya kushughulikia
masuala yasiyo ya Muungano katika Nchi Mshirika. Msingi huu utasaidia kuimarisha utendaji
katika muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa. 6.5 Vyombo vya kikatiba vinapendekezwa
kusimamia Misingi ya Utendaji Katika kuhakikisha kuwa Muungano unaimarika, Vyombo
vipya vya kikatiba vimependekezwa kusimamia Misingi ya Utendaji. Vyombo hivyo ni: (a)
Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali; (b) Mawaziri Wakaazi; (c) Mahakama
ya Juu; (d) Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
6.5.1 Tume ya
Uratibu na Uhusiano wa Serikali Tume ya Uratibu na Uhusiano wa Serikali inaanzishwa
na Ibara ya 109 na Makamu wa Rais atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Tume hii, na wajumbe
wake watakuwa ni Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar, Mawaziri Wakaazi na Waziri
mwenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tume hii, pamoja
na mambo mengine, itakuwa na dhima ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali
za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo na Serikali ya Muungano. Tume hii ambayo
inapendekezwa kuwa na Sekretarieti ya wataalam wa fani mbalimbali, itakuwa pia na
jukumu la kuwezesha uratibu na ushirikiano katika kutekeleza masharti yanayopendekezwa
na Rasimu ya Katiba, sera, sheria, mipango na mikakati baina ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali hizo.
6.5.2
Mawaziri Wakaazi Waziri Mkaazi ni nafasi ya madaraka inayopendekezwa na Ibara ya
67. Waziri Mkaazi atakuwa na wajibu wa kuratibu na kusimamia uhusiano baina ya Serikali
yake na Serikali nyingine ya Nchi Mshirika na kati ya Serikali yake na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano.
6.5.3 Mahakama ya Juu Mahakama ya Juu ni chombo
kingine kinachopendekezwa kuanzishwa katika Rasimu inayopendekezwa. Mahakama ya Juu,
pamoja na mambo mengine, inapendekezwa kuwa na mamlaka ya kushughulikia kusikiliza
na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika au baina ya Nchi Mshirika na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano. Mamlaka haya ya Mahakama ya Juu yanakusudia kusimamia misingi
ya utendaji katika muundo wa Muunganounaopendekezwa
6.5.4 Baraza
la Ulinzi na Usalama la Taifa. Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa linapendekezwa
kuanzishwa na Ibara ya 237 ya Rasimu inayopendekezwa. Baadhi ya Wajumbe wa Baraza
hilo litaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ni Makamu wa Rais, Rais wa Tanganyika
na Rais wa Zanzibar. Baraza hili litakuwa ndicho chombo pekee kitakachowakutanisha
Wakuu wa Serikali Tatu zinazopendekezwa na kitakuwa chombo cha juu cha kusimamia misingi
ya utendaji katika muundo wa Serikali unaopendekezwa.