Siku ya wapendanao kwa Mwaka 2014 yaaani we acha tu!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Februari 2014 Siku ya wapendanao anatarajiwa
majira ya mchana kukutana na kuzungumza na wanandoa watarajiwa kutoka sehemu mbali
mbali za dunia kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu
ya Maandali ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini
Vatican mwezi Oktoba mwaka huu.
Taarifa inaonesha
kwamba, wanandoa watarajiwa ni kutoka katika nchi ishirini na nane, hawa ni wale wanaotarajia
kufunga ndoa katika siku za usoni, ili kuhakikisha kwamba, upendo wao unadumu hadi
pale kifo kitakapowatenganisha kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu.
Sherehe
hizi za wapendanao zinatarajiwa kuanza majira ya saa 5: 00 kwa saa za Ulaya. Wanandoa
watarajiwa watashirikishana kwanza mambo msingi katika historia ya maisha yao ya upendo.
Saa 6:00 Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili uwanjani na kuanza kuzungumza na baadhi
ya wanandoa kuhusu: matatizo, changamoto, ubora wa maisha ya familia za Kikristo,
wajibu na dhamana ya kuchagua kuadhimisha Sakramenti ya ndoa Kanisani.
Kwa
bahati mbaya anasema, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia
baadhi ya wanandoa wamekuwa na tabia ya kuahilisha kufunga ndoa Kanisa kwa visingizio
vya matatizo na changamoto za maisha. Kuna haja ya kua na sera makini kuhusu maisha
ya ndoa na familia, kwa kutambua na kuheshimu dhamana ya maisha na utume wa ndoa katika
Jamii na Kanisa kwa ujumla.
Siku hii ya wapendanao, itakamilishwa kwa Sala
iliyotungwa na wanandoa watarajiwa na kila mmoja atapata zawadi maalum iliyoandaliwa
na Baba Mtakatifu Francisko kama kumbu kumbu ya Siku yao ya ndoa!