2014-02-13 14:54:22

Mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu ni kielelezo cha uhai wa Injili katika sayansi na tamaduni za watu


Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 14 Februari 2014 linafanya mkutano wake mkuu wa mwanzo wa Mwaka. Tarehe 12 Februari, limeendesha warsha ya siku moja kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Mchakato wa Uelimishaji leo na kesho".

Wajumbe wamepembua pamoja na mambo mengine kuhusu mabadiliko katika Waraka wa Kitume unaojadili kuhusu "Hekima ya Kikristo" sanjari na Maandalizi ya Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka kuhusu Elimu uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, sherehe ambazo zitafanyika Mwaka 2015. Sherehe hizi zinakwenda sanjari na kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Waraka wa Kichungaji kuhusu Elimu Katoliki; changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Uinjilishaji Mpya na mabadiliko ya kihistoria na kitamaduni yanayoendelea kujitokeza kwa kasi katika ulimwengu wa utandawazi.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Silku ya Alhamisi, tarehe 13 Februari 2014 amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano katika elimu kama sehemu ya mchakato unaopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, kila mtu ana haki ya kupata elimu, kwa kuzingatia uhuru wake, lakini Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo kama chimbuko la maisha, historia na ulimwengu katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu.

Baba Mtakatifu analitaka Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuhakikisha kwamba linawaandaa wataalam na mabingwa watakaojisadaka kwa ajili ya elimu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa kwa kutambua kwamba, utoaji wa elimu ni kitendo cha upendo na urithishaji wa maisha. Walimu wawe na ujuzi wa kuweza kuwamegea ujuzi na maarifa vijana wa kizazi kipya.

Walimu wanaotekeleza dhamana na utume wao katika vyuo na taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki hawana budi kuwa ni watu: wenye sifa, ujuzi na maarifa; watu wenye utajiri wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kwani vijana wanatamani kuona ushuhuda wa maisha ya walezi wao. Walimu waendelezwe katika taaluma ili waweze kuchangia kwa hali ya juu kuhusu weledi, imani na fadhila za maisha ya kiroho zilizoko ndani mwao!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Kanisa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mchango unaotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kama kielelezo cha uhai wa Injili katika sayansi na tamaduni za watu. Vyuo na Taasisi hizi zioneshe ukomavu na ujasiri wa kushindana na wadau wengine katika sekta ya elumu kwa kujenga utamaduni wa majadiliano pamoja na kutambua kwamba, wao wanamchango mkubwa wanaoweza kuwashirikisha pia walimwengu.

Baba Mtakatifu anasema, sekta ya elimu ni sawa na bahari kwani haina mwisho, Kanisa limekuwa daima mdau mkuu katika sekta ya elimu, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, elimu inashiriki kikamilifu katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wajumbe wa Baraza la Kipapa la Elimu kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu.







All the contents on this site are copyrighted ©.