2014-02-13 09:30:07

Kanisa Katoliki Uganda linaomboleza kifo cha Askofu Byabazaire, Baba wa Maskini!


Askofu Deogratias Muganwa Byabazaire wa Jimbo Katoliki Hoima, Uganda aliyefariki dunia hapo tarehe 8 Februari 2014 amezikwa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za Uganda, Jumanne tarehe 11 Februari 2014.

Ibada hii imehudhuriwa pia na Kardinali Emmanuel Wamala, Askofu mkuu Michael Blume, Balozi wa Vatican nchini Uganda pamoja na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Uganda. Marehemu Askofu Byabazaire anakumbukwa na wengi kutokana na unyenyekevu wake, huduma kwa maskini na wanyonge, kiasi kwamba, wengi walidiriki kumwita "Baba wa Maskini".

Ni kiongozi aliyejisadaka kuhakikisha kwamba, watoto wa maskini hata wao wanapata fursa ya kusoma vizuri kwani aliamini kwamba, elimu ni mkombozi wa wanyonge. Alijitahidi kuwa maskini kwa ajili ya kuwasaidia maskini, ingawa yeye mwenyewe alizaliwa katika familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, lakini hakumezwa na malimwengu, bali utajiri wote huu ulitumika kwa ajili ya mafao ya wengi Jimboni Hoima na Uganda katika ujumla wake.

Alionesha upendeleo wa pekee kwa wasichana kwa kuwajengea uwezo kwa njia ya elimu, ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo yao na yale ya Jamii inayowazunguka. Zaidi ya wasichana 300 walilipiwa ada na Marehemu Askofu Byabazaire. Ni kiongozi aliyeguswa na machungu ya watu wake, akawa tayari kuwalisha wenye njaa, kuwaganga waliovunjika moyo na kuwapatia matumaini na mwanga mpya wa maisha, wale wote waliotembea katika giza la utupu wa maisha!

Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, katika salam zake za rambi rambi anasema, Kanisa Katoliki Uganda limempoteza mchungaji mwema, aliyejisadaka kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa nchini Uganda, atakumbukwa kutokana na tabasamu, ucheshi na ukarimu kwa wote aliokutana nao katika hija ya maisha yake hapa duniani. Alijikita katika kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.

Baada ya kujenga shule, alikuwa na mkakati wa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Bunyoro. Kwa hakika Askofu Deogratias Muganwa Byabazaire alijipambanua zaidi kutokana na upendo wake kwa Mungu na jirani!

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Askofu Byabazaire alizaliwa huko Kajurubu-Masindi, Jimbo Katoliki la Hoima tarehe 9 Oktoba 1941. Akapadrishwa tarehe 9 Agosti 1969. tarehe 21 Mei 1990 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki la Hoima. Tarehe 9 Machi 1991 akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Hoima, Uganda. Amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.







All the contents on this site are copyrighted ©.