2014-02-12 11:49:08

Siku ya Wapendanao! Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kutimua vumbi!


Katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendanao, hapo Ijumaa tarehe 14 Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wanandoa watarajiwa wapatao ishirini elfu wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Ndoa Takatifu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hizi ni juhudi za Baraza la Kipapa la Familia kama sehemu ya Maandalizi ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu Familia, itakayofanyika mwezi Oktoba hapa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara nyingi amewataka wachumba na wanandoa watarajiwa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao upendo wa dhati na furaha ya maisha ya unyumba yanayojikita katika utakatifu wa maisha, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, pamoja na kumkaribisha Yesu katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anasema, Sakramenti ya Ndoa ni wito mtakatifu na agano ambalo kwa njia yake mwanaume na mwanamke huunda kati yao Jumuiya kwa maisha yao yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Hili ni agano ambalo Kristo mwenyewe amelikuza na kulipatia hadhi ya kuwa ni kati ya Sakramenti za huduma. Wanandoa hawana sababu ya msingi ya kutojisadaka kwa ajili ya wenzi wao, kwani kwa pamoja wanaweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa njia ya imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu anasema, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa vijana wa kizazi kipya zinakabiliwa na changamoto kubwa. Hii inatokana na ukweli kwamba, vijana wengi wamemezwa na malimwengu, ubinafsi unatawala na wakati mwingine hawana msingi thabiti wa maisha ya kiroho na kiutu. Huu ni utamaduni wa ubinafsi unaoshindwa kuonesha upendo wa dhati kwa mwenzi wa ndoa.

Mama Kanisa kwa kutambua changamoto hizi, anaendelea kujikita katika maandalizi makini ya wanandoa watarajiwa pamoja na kuwapatia majiundo endelevu baada ya kufunga ndoa, ili waweze kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo maisha ya: sala, upendo na ukarimu yanamwilishwa katika uhalisia wake. Vyama vya kitume Parokiani ni tunu msingi katika mchakato wa kuwasaidia wanandoa wapya kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alitoa kipaumbele cha pekee kwa familia na kutaka kuwe'po na maandalizi ya kutosha kabla ya waamini hawajafunga ndoa, ili kweli ndoa na maisha ya kifamilia yawe ni sehemu ya hija ya utakatifu wa maisha. Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita aliwahi kusema kwamba, wanandoa wanapaswa kumpatia Yesu kipaumbele cha kwanza katika maisha yao ya kila siku, kwa wanandoa kuishi kwa ukamilifu na uaminifu ahadi zao za ndoa kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao.

Wanandoa watarajiwa wajitahidi kufahamiana zaidi kwa kufanya tafakari ya kina na hatimaye, kufanya uamuzi wenye ukomavu, unaodumu hadi kifo kitakapowatenganisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.