Mradi wa miaka 5 kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi wazinduliwa
nchini Tanzania
Mfuko wa Msamaria mwema, unaosimamiwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji
kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kushirikiana na Idara ya afya ya Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania na Kampuni ya Gilead Sciences kutoka Marekani, wamekubaliana
kimsingi kusaidia juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi mkoani Shinyanga, kwa kusaidia
juhudi za kupima virusi vya Ukimwi kwa wananchi 120, 000 pamoja na kuwapatia dawa
za kurefusha maisha wale watakaokuwa wameathirika.
Makubaliano hayo yamefikiwa
Jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Februari 2014 katika Maadhimisho ya Siku ya 22 ya
Wagonjwa Duniani. Huu ni mradi wa miaka mitano kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi
na kutoa dawa za kurefusha maisha. Ni mradi unaozingatia taaluma, maadili, usafi pamoja
na mafunzo kwa walengwa watakaofaidika na mradi huu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa watoto yatima.
Mradi huu utaendelea kuongeza nguvu katika kuwahudumia
wagonjwa wa Ukimwi, juhudi zinazofanywa na Jimbo Katoliki la Shinyanga katika Vituo
vya Afya vya: Ngokolo, Bugisi, Buhangija na Mija. Mradi utatoa ufadhili kwa ajili
ya mafunzo ya hali ya juu kwa wahudumu wa sekta ya afya, ili kuweza kutekeleza wajibu
wao barabara pamoja na kuendelea kujikita katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi
na maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto.
Wananchi watakaogundulika kuwa
na maambukizi ya Ukimwi watapewa dawa za kurefusha maisha anasema Askofu mkuu Zygmunt
Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika
sekta ya afya. Mradi unapania pamoja na mambo mengine, kudhibiti maambukizi ya virusi
kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, kama sehemu ya huduma makini inayotolewa na Kanisa
katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kama sehemu ya mwendelezo wa agizo
la Kristo katika kuwahudumia wagonjwa.
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, amemkumbuka
kwa namna ya pekee, Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, aliyefariki
dunia mwezi Novemba 2012. Aliamini kuhusu mafanikio ya mradi huu katika kuwahudumia
watanzania waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Ni mradi wa pekee, unaojumuisha
Mfuko wa Msamaria Mwema, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi
katika sekta ya afya pamoja na Kampuni ya Gilead.
Lengo li kuhakikisha kwamba,
Kanisa Katoliki linashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi
ambao umekuwa ni chanzo cha vifo na upotevu wa nguvu kazi nchini Tanzania.
Maadhimisho
ya Siku ya Wagonjwa Duniani, yalianzishwa kunako mwaka 1992 na Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili, ambaye hapo tarehe 27 Aprili 2014 anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu.
Siku ya Wagonjwa Duniani inalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, wagonjwa
wanapata huduma bora pamoja na kuishirikisha Familia ya Mungu katika huduma kwa wagonjwa,
kwani wagonjwa bado wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa.
Kanisa
linawahamasisha watu wa kujitolea, ili waweze kuwashirikisha jirani zao upendo, kwa
kuwaonjesha upendo. Kanisa linapania pia kutoa majiundo makini ya kitaaluma na kimaadili
kwa wahudumu wa sekta ya afya.