Changamoto za maisha ya kiroho na kiutu nchini Bulgaria baada ya kuanguka kwa utawala
wa Kikomunisti!
Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgaria linaanza hija yake ya kitume mjini Vatican kuanzia
tarehe 13 hadi tarehe 15 Februari 2014. Hili ni Kanisa dogo lakini lenye umuhimu wa
pekee, kwani waamini wa Kanisa Katoliki nchini Bulgaria wanaunda asilimia 1.1% ya
idadi ya wananchi wote wa Bulgaria.
Kuna majimbo matatu yaliyoundwa kunako
mwaka 1995 na Maaskofu wake wote ni wale walionja "chungu" ya utawala wa Kikomunisti.
Kanisa nchini Bulgaria linaendelea kukabiliana na changamoto za ukanimungu, kwa kujikita
zaidi na zaidi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya Furaha. Kanisa limejiwekea
mikakati ya kuwahamasisha waamini kuhusiana na masuala ya maisha ya kiroho na kiimani
baada ya kukosa uhuru wa kidini kwa miaka mingi chini ya utawala wa Kikomunisti. Familia
inaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali kutoka ndani na nje ya familia zenyewe.
Ndoa nyingi hazina misingi thabiti ya imani, kiasi kwamba, zinaendelea kuvunjika
hata katika uchanga wake. Uchumba sugu ni kati ya mambo yanayokwamisha ndoa za Kikristo
anasema Askofu Christo Proykov, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgaria. Vijana
nchini Bulgaria baada ya kufungua macho kwa njia ya mitandao ya kijamii na njia za
mawasiliano, wanapenda kuiga kila kitu kinachopita machoni mwao, hatari kubwa ni kuona
kwamba, vijana hawa wanajikuta wakikabiliana na athari za kumong'onyoka kwa maadili
na utu wema.
Maaskofu Katoliki Bulgaria wanaendelea kujiandaa kikamilifu kwa
ajili ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa
mwezi Oktoba, 2014 hapa mjini Vatican. Kuna umoja na mshikamano wa kidugu na kiimani
kati ya waamini wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox nchini Bulgaria. Wanaendelea
kuwa macho na makini kwa Mafundisho Tanzu ya Kanisa, lakini bado wanahitaji majiundo
endelevu ili kuweza kukabiliana na changamoto katika maisha ya kiimani.
Waamini
wanapaswa kutambua umuhimu wa Makanisa mahalia katika ujenzi wa mshikamano wa upendo
na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na athari za myumbo
wa uchumi kimataifa. Kanisa nchini Bulgaria linajielekeza zaidi katika matumizi ya
njia za mawasiliano ya kijamii kwa ajili ya utangazaji wa Injili ya Furaha miongoni
mwa wananchi wa Bulgaria.
Wananchi wengi wa Bulgaria wamempokea na kumkubali
Papa Francisko kutokana na mtindo wake wa maisha, lakini zaidi kwa kuguswa na mahangaiko
ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Maaskofu wa Bulgaria walipata
fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa wana furaha
ya kukutana na Papa Francisko ili kuweza kusikiliza ushauri wake kutokana na changamoto
wanazokabiliana nazo katika medani mbali mbali za maisha, ili kusonga mbele kwa imani
na matumaini makubwa zaidi.
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yamekuwa ni fursa
kubwa kwa waamini nchini Bulgaria kutambua na kuheshimu zawadi ya imani waliyoipokea
kutokana na Sakramenti ya Ubatizo. Imani ni kielelezo cha maisha, ni nguvu na mwanga
thabiti. Waamini wanaendelea kuchangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha
wengine imani yao pamoja na kuitolea ushuhuda, kwani watu wengi wanavutwa zaidi na
ushuhuda wa imani tendaji, kielelezo cha wokovu, ukweli na furaha ya maisha. Kimsingi,
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, limekuwa ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu kwa
waamini wa Kanisa Katoliki nchini Bulgaria.
Askofu Christo Proykov anasema
kwa kutambua na kuthamini maisha ya ndoa na familia sanjari na maandalizi ya Maadhimisho
ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Bulgaria
limeutangaza Mwaka 2014 kuwa ni Mwaka wa Familia. Kila siku mara baada ya Maadhimisho
ya Fumbo la Ekaristi, waamini wanasali kwa ajili ya kuombea familia.
Waamini
wanaendelea kufundishwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango
wa Mungu. Bado kuna haja ya kujikita katika majiundo makini ya waamini kuhusiana na
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa.