2014-02-11 07:51:58

Msikumbatie utamaduni wa kifo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linapinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za kifo laini kwa kusema kwamba, mtu anaweza kuaga dunia kwa heshima huku zawadi ya maisha, ikiheshimiwa na wala si kwa kuhalalisha sera za kifo laini kwa kutumia mgongo wa sheria za nchi. Hili ni jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. RealAudioMP3

Serikali ya Ubelgiji hivi karibuni ilipitisha sheria ya kifo laini kwa watoto wadogo, ikiwa kama wazazi watapata idhini kutoka kwa mwanasaikolojia kama sehemu ya mchakato wa kumwondolea mtoto maumivu au mateso kutokana na magonjwa yasiyokuwa na tiba muafaka au pale mtoto anapoelekea kufani. Kifo laini kinaweza kutekelezwa kwa kutumia timu ya madaktari baada ya kupata ridhaa ya wazazi. Maaskofu Katoliki nchini Ubelgiji wanauliza swali la msingi, imekuwaje, Serikali kuamua kujichukulia dhamana ya kusitisha maisha ya raia wake kwa njia ya sheria?

Sheria hii ni nyeti kutokana na ukweli kwamba, athari zake zinaweza kuenea hata kwa wagonjwa wengine kama: watu wenye ulemavu, magonjwa ya afya ya akili na hata wale ambao wamechoka kuishi na maisha kwao hayana tena mashiko wala thamani. Maaskofu wanasema sheria hii inaonekana kumjali mtu anapokuwa mzima na anapokuwa anaweza kuchangia na kwamba utu na thamani yake kama binadamu vinapimwa kwa kigezo cha uwezo wake wa kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi na kwamba, maisha hayana tena thamani kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wananchi hawana budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi ya tiba ya mwanadamu, kuna matibabu yanayoweza kutolewa kwa ajili ya kutuliza maumivu makali na matibabu yanayomwandaa mgonjwa kulipokea fumbo la kifo kwa heshima kubwa.

Kuna haja kwa wananchi kuendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu Maisha na Fumbo la Kifo kwa binadamu. Kila mwanadamu ana uhakika kwamba, iko siku moja atafariki dunia, lakini mtu anaweza kuifikia siku hii kwa kulinda na kuthamini utu, heshima na maisha ya binadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana na jukumu la madaktari kumwondolea mgonjwa maumivu na kero nyingine za maisha, lakini pia mgonjwa pamoja na familia yake wanapaswa kusaidiwa kupokea ugonjwa katika hali ya utulivu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linasema kwamba, sheria ya kifo laini au eutanasia inachezea maisha ya mwanadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mateso na kifo kwa mwamini yanapata maana yake ya pekee katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linawaalika waamini, watu wenye mapenzi mema pamoja na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kuzingatia kanuni maadili katika kukabiliana na changamoto hii.








All the contents on this site are copyrighted ©.