2014-02-11 07:43:24

Misimamo mikali ya kidini ni changamoto inayopaswa kuangaliwa kwa mapana, ili kujenga moyo wa majadiliano ya kweli!


Askofu Bernadin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, Tanzania anaadhimisha miaka mitatu tangu alipoteuliwa kuliongoza Jimbo Katoliki la Kondoa, ambalo ni kati ya majimbo 34 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Tanzania, lenye idadi ya waamini wapatao millioni 9, sawa na asilimi 20% ya idadi ya wananchi wote wa Tanzania. RealAudioMP3

Wakristo kwa pamoja ni asilimia 30 ya idadi ya watanzania wote. Waislam ni sawa na asilimia 35% na watanzania wengine ni wale ambao bado wanajikita katika imani zao za jadi. Kwa miaka mingi, Tanzania ilihesabiwa kuwa ni kati ya nchi zilizokuwa zinajikita katika misingi ya Amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, kazi kubwa iliyofanywa na Baba wa Taifa, Mwalim Julius Kambarage Nyerere, lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumeanza kuonekana dalili za mpasuko kwa kuporomoka kwa misingi ya Amani na mshikamano wa kitaifa.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania hivi karibuni limeadhimisha Jubilee ya Miaka 150 ya Uinjilishaji endelevu Visiwani Zanzibar, mahali ambako kuna idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. Kwa miaka mingi wananchi wa Zanzibar waliishi kwa Amani, upendo na mshikamano, lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumeibuka kundi la waamini wenye msimamo mkali wa kiimani, hali inayotishia Amani, ustawi na maendeleo ya Tanzania katika ujumla wake.

Tatizo la misimamo mikali ya kiimani anasema Askofu Bernadin Mfumbusa linapaswa kueleweka katika mitazo mikuu mitatu, kwanza: kuna baadhi ya wananchi Zanzibar wanadai kwamba, dini ya Kiislam ndiyo dini ya Serikali ya Zanzibar, kinyume cha Katiba ya Nchi, kwani Serikali kimsingi haina dini, bali wananchi wake wana dini na imani zao. Pili, misimamo mikali ya kiimani ni mwelekeo wa kimataifa unaoigusa na kuvitikisa Visiwa vya Zanzibar.

Tatu, masuala ya kisiasa Visiwani Zanzibar yanapambwa na udini, kwa kutaka kuwasadikisha kwamba, wao ndio watetezi wa tunu msingi za maisha ya kiroho miongoni mwa waamini wa dini ya Kiislam. Lakini ikumbukwe kwamba, wananchi wengi wa Zanzibar wanataka kuishi kwa kuendelea kujenga na kudumisha misingi ya amani na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Wasi wasi wa vitendo vya kigaidi vinavyoweza kufanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani ipo nchini Tanzania kama ilivyo hata kwa sehemu nyingine ya dunia anasema Askofu Mfumbusa katika mahojiano maalum na Shirika la Kipapa la Makanisa hitaji. Kuna baadhi ya sehemu kama vile Tanga, harufu ya vitendo vya kigaidi ilianza kunukia. Kundi hili ni lile la watu wanaopelekwa nje ya nchi na kupata mafunzo huko na baadaye kurudi nchini Tanzania ili kuvuga wananchi. Vikundi hivi ni kama kile cha Uamsho kilichotikisa Visiwani Zanzibar kwa matukio ya kutisha pamoja na kusababisha kinzani za kidini zilizopelekea maafa na uharibifu mkubwa wa majengo ya Ibada.

Askofu Mfumbusa katika mahojiano haya anaonya kwamba, watu wasichukulie mambo juu kwa juu kama “mkungu wa ndizi”, bali watambue kwamba, kuna kundi kubwa la waamini wa dini ya Kiislam ambao ni wapenda na wajenzi wa amani, kama ilivyo pia kwa Wakristo. Jambo la msingi ni kuendelea kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini, kuheshimiana na kuthaminiana sanjari na kutambua tofauti za kiimani zilizopo; mambo ambayo kwa pamoja yanapaswa kuwa ni kielelezo cha utajiri mkubwa na urithi wa watanzania wote.

Askofu Mfumbusa anasema chuki za kidini kati ya Waislam na Wakristo zinajikita katika madai kwamba, Waislam wamekuwa wakinyanyaswa na kudhulumiwa na Wakristo kwa miaka mingi; madai ambayo yamesikika hata huko Jamhuri ya Wananchi wa Afrika ya Kati na hata Tanzania katika ujumla wake. Lakini huu si ukweli wa mambo, Wakristo wanatumiwa tu kuficha ukweli wa mambo.

Wakristo kwa upande wao, wataendelea kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano ya kidini, katika misingi ya ukweli na uwazi; upendo na msamaha. Tatizo la misimamo mikali ya kidini haliwezi kutatuliwa kwa sera na falsafa ya “jino kwa jino au jicho kwa jicho” kwani hii ni hatari. Ni majadiliano yanayojikita katika huduma msingi za kijamii kama vile katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu yanayopaswa kutolewa bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile!

Askofu Mfumbusa anasema, uwepo wa dhambi na maovu ni sehemu ya ubinadamu, ndiyo maana watu wanaendelea kuathirika kutokana na vita, chuki na uhasama. Bado anakumbuka mauaji ya Padre Ambroce Mkenda aliyeuwawa Jimboni Zanzibar kwani alikuwa ni mwanadarasa wake Seminari ndogo kwenye miaka 1980.

Askofu Mfumbusa akijibu swali kuhusu upweke wa maisha ya Kiaskofu anasema kwamba, huu ni ukweli usiofumbiwa macho, kwani kama Askofu wa Jimbo kuna mambo ambayo anapaswa kuyatolea maamuzi. Bado kuna idadi ndogo ya Mapadre Jimboni mwake wanaohudumia kundi na eneo kubwa Jimboni Kondoa. Barani Afrika maisha ya Kijumuiya ni sehemu ya vinasaba vya watu wake, kumbe hata katika kile kinachoweza kuonekana kuwa ni upweke, bado anazungukwa na umati mkubwa wa waamini na majirani wema.

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Kondoa ina nafasi ya kumtembelea wakati wowote anapokuwa na nafasi kwani huu ni utajiri wa mila na tamaduni njema za Kiafrika. “Mgeni ni mafuta ya jumuiya”. Katika sala na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa anaonja uwepo wa Kristo mwenyewe katika hija na utume wa maisha yake.

Askofu Mfumbusa anasema, miito ya Kipadre na Kitawa nchini Tanzania inaendelea kuongezeka kwa kasi nzuri. Hadi sasa kuna zaidi ya Mafrateri 500 wanaoendelea na majiundo yao ya Kikasisi huko kwenye Falsafa na Taalimungu. Kuna baadhi ya watu wanaaamua kujiunga na maisha ya Kipadre na Kitawa wakiwa na umri mkubwa! Pengine kuna haja ya kufanya utafiti wa jambo hili kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Tanzania.

Umoja na mshikamano wa kidugu ni kati ya vinasaba vya utambulisho wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Ni utajiri unaovuka mipaka ya ukabila, umajimbo na mahali anapotoka mtu. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na kielelezo cha imani tendaji ni kati ya mambo yanayoendelea kutoa utambulisho wa Kanisa mahalia nchini Tanzania.

Askofu Mfumbusa anasema kati ya mambo yanayompandisha “BP” kwa Mwaka 2014 ni idadi ndogo ya Mapadre. Kwa sasa Jimbo Katoliki la Kondoa lina jumla ya Mapadre 13 wanaohudumia Parokia 11. Kwa sasa Jimbo Katoliki la Kondoa lina mpango wa kufungua Parokia sita kwa mpigo! Lakini uhaba wa Mapadre unakwamisha mchakato huu. Angependa kuhakikisha kwamba, anakuwa na kikosi kazi kwa ajili ya majiundo ya vijana walioko Sekondari na Taasisi za elimu ya Juu.

Makatekista na waamini walei wanapaswa kujengewa uwezo ili kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Tanzania katika sekta ya elimu. Kuna haja ya kufanya maboresho kwenye Seminari kuu za Tanzania kwa kuongeza vitabu vya kiada pamoja na mitandao ili Majandokasisi waweze kujielimisha zaidi kwa kutumia pia njia za mawasiliano ya kisasa.

Jimbo Katoliki Kondoa linaendelea kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hadi sasa kuna Kituo cha kulelea Watoto Yatima wapatao 70: kuna Kituo cha Afya na Zahanati zilizoenea kwenye Vijiji mbali mbali. Askofu Bernadin Francis Mfumbusa anasema, Jimbo Katoliki la Kondoa lingependa kufanya mengi, lakini rasilimali watu na fedha ndilo tatizo kubwa kwa wakati huu!

Habari hii imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.