2014-02-10 08:15:50

Waonjesheni wagonjwa: imani na mshikamano wa upendo!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita, tarehe 9 Februari 2014 amewakumbusha waamini kwamba, Tarehe 11 Februari, 2014, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani ambayo kwa Mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu "Imani na Upendo: imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu". RealAudioMP3

Siku ya Wagonjwa Duniani ni mwaliko na changamoto kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa wagonjwa kwa kuwaonjesha upendo na ukarimu, daima wakijitahidi kumuiga Kristo aliyeguswa na mahangaiko ya wagonjwa mbali mbali. Yesu anataka kuwaponya na kuwafariji kwa kuwafunguliwa moyo wake unaobubujika matumaini.

Baba Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kazi njema wanayofanya kwa ajili ya wagonjwa, watu ambao wanahitaji kuonjeshwa ukarimu na matatizo yao kupewa majibu muafaka. Hata katika taabu na mahangaiko ya ugonjwa wake, mgonjwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote wanaoteseka kwa ajili ya magonjwa mbali mbali kwamba, yuko pamoja nao katika sala zake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kusaidiana kwa hali na mali katika kukabiliana na magonjwa mbali mbali na kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii pia kutuma salam zake za kheri na pongezi kwa viongozi na wanamichezo kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshiriki katika michezo ya Olympic Kipindi cha Baridi huko Russia, kuhakikisha kwamba, michezo inakuwa ni kielelezo cha sherehe na urafiki.

Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wote wanaoendelea kuteseka kutokana na maafa asilia sehemu mbali mbali za dunia, watambue kwamba, yuko karibu nao kwa njia ya sala zake. Majanga asilia ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu; daima wakiwa makini kulinda na kutunza mazingira na pale inapowezekana, jitihada za makusudi zifanyike ili kuzuia maafa asilia. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni amewataka waamini kuwa ni chumvi na mwanga kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.