2014-02-10 07:50:52

Wakristo wanapaswa kuwa ni chumvi na mwanga wa dunia!


Mkiwa maskini wa roho, wenye huzuni, wapole, wenye njaa na kiu ya haki, wenye rehema, wenye moyo safi na wapatanishi, mtakuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia. Ni maneno ya Yesu mwenyewe kwa mitume wake mara baada ya kuwapatia muhtasari wa mafundisho yake makuu yanayofumbatwa katika heri za Mlimani.

Itakumbukwa kwamba, mitume walikuwa ni watu wa kawaida kabisa waliotwaliwa miongoni mwa wavuvi ili kushiriki katika azma ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Chumvi kwa Waisraeli ilikuwa ni alama ya kunogesha agano kati ya Mungu na Waisraeli na kwamba, mwanga ni alama ya ushindi wa Masiha ambaye anakuja kulifukuza giza katika maisha ya watu.

Ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita tarehe 9 Februari 2014, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Wakristo ni kielelezo cha Waisraeli wapya katika Agano Jipya ambao wamepokea dhamana na utume unaofumbatwa katika imani na mapendo, ili waweze kutoa mwelekeo mpya, wawabariki na kuwawezesha wanadamu kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Kila Mkristo ni mtume na mmissionari anayetumwa ulimwenguni ili kuwa kweli ni Injili Hai inayojionesha katika maisha matakatifu ili kutoa ladha katika medani mbali mbali za maisha dhidi ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi. Kwa njia ya maisha matakatifu, waamini wanaweza kuwa ni mashahidi wa mwanga wa Kristo unaojikita katika fadhila ya upendo. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia, dhamana waliyoipokea kutoka kwa Kristo mwenyewe.

Waamini waendelee kuwa ni mwanga ambao ni zawadi inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ikiwa kama mwamini atauzima mwanga huu, maisha yake yatakosa dira na mwelekeo. Daima wahakikishe kwamba, maisha yao ni taa inayowaka na kuonekana na watu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili, kwani ni mwanga kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao waamini wanapaswa pia kuwashirikisha wengine. Huu ndio wito wa kila Mkristo anasema Baba Mtakatifu Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.