2014-02-10 11:11:49

Wahudumieni watu kwa moyo wa upendo, ili waonje huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake!


Waamini wanahamasishwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha, Matumaini na Upendo, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yanayojikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hakuna sababu ya kutaka kuwaongoa watu kuingia katika Ukristo kwa nguvu, bali wao wenyewe wavutwe kutokana na ukarimu na upendo unaojionesha miongoni mwa Wakristo katika huduma na maisha adili.

Hayo yamesemwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam katika ufunguzi wa Kliniki ya Upasuaji kwa ajili ya Watoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, iliyoko Manyoni, Singida, Tanzania. Anasema, Injili ya kweli inajikita katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, na hii ndio maana ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kardinali Pengo amewashukuru na kuwapongeza Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania kwa ushiriki wao katika kuwahudumia watanzania katika sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu. Wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika sekta ya afya kwa kuendeleza utume ulioanzishwa na Kristo mganga mkuu wa kuwaponya watu magonjwa yao pamoja na kuwaondolea dhambi zao.

Kardinali Pengo amewataka wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanajituma bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa: kwa kuzingatia: maadili ya kazi, weledi, utu na heshima ya binadamu. Wagonjwa hata katika magonjwa yao bado wanaendelea kubaki na chapa ya sura na mfano wa Mungu katika maisha yao, hivyo wathaminiwe, waheshimiwe na kupendwa kama Kristo mwenyewe alivyowapenda na kuwahudumia.

Amewataka wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Tanzania kutojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kwani ni kinyume cha haki msingi za binadamu na kielelezo cha kumong'onyoka kwa maadili na utu wema. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali Polycarp Pengo alikuwa Singida kwa ajili ya kushiriki katika ufunguzi wa Kliniki ya Upasuaji wa watoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Tanzania. Ujumbe kutoka Vatican ulioongozwa na Professa Giuseppe Profiti, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ambayo imechangia jumla ya shilingi millioni mia tano na ishirini na tano pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya huduma ya upasuaji kwa watoto wadogo nchini Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.