2014-02-10 08:25:29

Vipingamizi au vizuizi vya ndoa ya Kikristo!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu pendevu cha Kanisa la nyumbani, karibu katika mwendelezo kipindi chetu cha kanisa la nyumbani. Ili twende pamoja, tukumbuke msingi, tunapozungumzia Kanisa la Nyumbani, twamaanisha familia. Tunapozungumzia familia kadiri ya imani na maadili yetu ya kikatoliki, tunamaanisha baba, mama na watoto. RealAudioMP3
Lengo letu: tusaidiane kuzijenga vema familia zetu, ili ziwe chimbuko la watu wanaofaa kwa ajili ya Utukufu wa Mungu na ujenzi wa Kanisa na utumishi kwa familia nzima ya mwanadamu.

Katika kipindi kilichopita tuliangazia wajibu wetu kama jamii katika kuwasaidia wanandoa waanzaji au wanandoa changa, waweze kuanza maisha yao ya umoja na upamoja kwa mwondoko wenye matumaini tele. Tuhitimishe tafakari ile kwa kutoa rai ya jumla kwamba “kila mmoja ajiwekee nidhamu binafsi, ili kwa mawazo, kauli au matendo asiwe sababu ya kuyumbisha ndoa na familia za wengine”.

Hii nidhamu binafsi ijengwe katika dhamira safi na hofu ya Mungu. Usipojiwekea nidhamu katika hilo na kulisimamia wewe mwenyewe, yule mwovu anaweza akakubinafsisha, akakutumia wewe kama ndiyo nyundo ya kuponda ndoa za watu na hivyo kuyumbisha kabisa usitawi wa Kanisa kwa ujumla. Haitapita siku au wiki haujaleta uvundo katika ndoa za watu.

Katika kipindi hiki, tunatoa utangulizi kwa vipindi vichache vijavyo, ambavyo tutazungumzia juu ya “vipingamizi au vizuizi vya ndoa”. Bila shaka wengi tutakuwa tunasikia makanisani yanaposomwa matangazo ya ndoa tunaambiwa ‘anayejua kizuizi apelekea habari katika ofisi ya Paroko’. Mara nyingine wengi wetu hatufahamu hivyo vizuizi, hata kama vipo tunakaa kimya. Halafu shida ikianza kuonekana baadaye unasema ‘mimi nilijua ila nilikaa kimya tu’! Haifai!. Katika makala hizi tutapeana maarifa mepesi ya hivyo vizuizi kadiri ya sheria ya Kanisa.

Kwa nini Kanisa lizungumzie vizuizi vya ndoa?
Kanisa aliye mama na mwalimu wa watu wote kwa wakati wote (re. KKK 2030-2033), daima anaheshimu na kujali sana taasisi ya ndoa kama wito muhimu ambamo kutoka kwamo Kanisa linajengwa. Kuanzia mwanzo anaweka taratibu-kanuni zenye kuratibisha masuala yote yahusuyo maisha ya ndoa na familia likiwa na lengo la kuimarisha misingi. Kanisa linaamini kwa dhati kwamba, usitawi wa jamii adilifu huchangiwa vikubwa kabisa na usitawi wa ndoa na familia bora.

Hivyo, katika kuchangia usitawi huo, Kanisa linatoa miongozo inayomsaidia kila mmoja wetu kutambua na kuthamini wito huu, na zaidi kuwasaidia wote wenye kuitika wito huo, watambue na waupokee wajibu msingi yaani kuzaa watoto na kuwatunza (uzazi mwajibifu), na waweze pia kudumisha furaha yao wao wenyewe. Kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Kanuni-Kanuni zetu, Kanisa la nyumbani lijengwe kwa unadhifu wote na kutoka humo Mama Kanisa ajipatie watoto wengi zaidi wa ufalme.

Tangu mwanzo kabisa wote tujue kuwa ndoa ni Sakramenti kati ya Sakramenti saba za Kanisa. Na sakramenti ni alama wazi zilizowekwa na Yesu Kristo mwenyewe ili zitupatie neema za wokovu. Na katika kuadhimisha kila sakramenti, kuna mafaa mawili makubwa yanatokea kwa wakati huohuo, yaani: Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa. Hapo Kanisa linafundisha, agano la ndoa linawatakatifuza wanandoa wenyewe na kumpa Mungu utukufu Mkuu (Kwa habari ya Kanisa na Sakramenti ya ndoa tusome KKK 1062 – 1666).

Sakramenti ya ndoa ni wito ambao mwasisi wake ni Mungu mwenyewe (Mw. 1:26-28). Katika wito huo wa ndoa, MTU MUME NA MTU MKE wanawekeana maagano ya maisha mbele ya Mungu na Kanisa lake, wanaapiana kupenda, kuheshimiana nyakati zote na kwa hali zote za maisha yao ya hapa duniani. Wanaahidi na kuapa kutekeleza wajibu wa kuwapoke na kuwatunza watoto kama ilivyo SHERIA YA KRISTO NA KANISA LAKE. Kwa sasa, tena kwa makusudi makubwa tunapenda kusisitiza, KADIRI YA MPANGO WA MUNGU, NDOA NI YA MTU MUME NA MTU MKE, na siyo vinginevyo (Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja". Mwanzo 2:24).

Kanisa linaweka taratibu Kanuni za kuratibisha maisha ya ndoa, ili kusaidia malengo hayo yatimilike na mafaa hayo yatukie. Kwa mujibu wa sheria ya Kanisa, tuna vizuizi kumi na viwili vya ndoa. Vizuizi vya ndoa, ni jumla ya mambo yote yanayoweza kuathiri uhalali wa agano la ndoa, na hivyo kwa namna moja au nyingine kuzuia malengo na mafaa ya agano la ndoa. Katika kipindi kijacho tutavitazama hivyo vizuizi vya ndoa.

Tunaahirisha kipindi chetu cha leo kwa kuimarishwa na neno la Mungu asemapo “Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu”. Kutoka katika studio za Radio Vatican, hadi wakati mwingine, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.