2014-02-10 12:00:44

Mheshimiwa Padre Moses Hamungole mkuu wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Monze, Zambia


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Emilio Patriarca wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia ya kung'atuka kutoka madarakani kadiri ya sheria za Kanisa namba 401ยง1. Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Moses Hamungole kutoka Jimbo kuu la Lusaka Zambia kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Monze. Hadi kuteuliwa kwake Padre Moses Hamungole alikuwa ni mkuu wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican.

Askofu mteule Moses Hamungole alizaliwa kunako Mei, Mosi, 1967 Jimbo kuu la Lusaka, Zambia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 6 Agosti 1994 kwa ajili ya Jimbo kuu la Lusaka, Zambia. Baada ya upadrisho ametekeleza utume wake kama Paroko msaidizi kwenye Parokia za New Kanyama, Railway- Chowa. Aliwahi pia kuwa ni Mkurugenzi wa Radio Yatsin na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Jimbo kuu la Lusaka.

Baada ya masomo yake ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani, kunako Mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alikuwa ni Katibu wa Idara ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kwenye Makao yake Makuu yaliyoko mjini Nairobi. Kati ya Mwaka 2002 hadi Mwaka 2009 alikuwa ni Rais wa Signis Afrika.

Kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2010 alijiendeleza zaidi katika masomo ya uzamivu katika fani ya mawasiliano ya Jamii, Chuo Kikuu cha Leuven, nchini Ubelgiji. Tangu Mwaka 2010 hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni mkuu wa Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican. Wafanyakazi na wadau wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican wanamtakia kheri na baraka tele Askofu mteule Moses Hamungole kwa dhamana na wajibu huu mpya aliokabidhiwa na Mama Kanisa kwa sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.