2014-02-08 08:11:25

Waonjesheni watoto wema, upendo na ukarimu ili kulinusuru taifa kutoka katika mmong'onyoko wa maadili na utu wema!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Ijumaa tarehe 7 Februari 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya ufunguzi wa Kliniki ya Upasuaji wa Watoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Tanzania.

Ujenzi wa Kliniki ya Upasuaji wa Watoto ni kielelezo cha mshikamano wa upendo na kidugu kutoka Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Katika mahubiri yake, Kardinali Pengo amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha utamaduni wa kuwapenda na kuwajali watoto katika maisha na malezi yao, ili waweze kuona kwamba, dunia kweli ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kardinali Pengo anasema, ukatili, nyanyaso na madhulumu yanayofanywa dhidi ya watoto wadogo kwa kukumbatia: utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba na nyanyaso kwa watoto, vimekuwa ni chanzo kikubwa kwa mmong'onyoko wa maadili na utu wema miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kiasi cha kuwakatisha tamaa na hivyo kukosa dira na mwelekeo wa maisha. Matokeo yake ni vijana hawa kujitumbukiza katika vitendo vya jinai, ulevi, matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo.

Haya ni matukio yanayofanywa na vijana kiasi cha kuwafanya watu wengi ndani ya Jamii kushikwa na bumbuwazi na kuanza kujiuliza haya yote yametoka wapi? Anasema Kardinali Pengo! Jamii inapaswa kujenga fadhila na utamaduni wa kuwapenda, kuwathamini na kuwajali watoto, kama alivyofanya Yesu mwenyewe, kwa kuonesha upendeleo wa pekee kwa watoto wadogo, ili kuondokana na tatizo la kumong'onyoka kwa maadili na utu wema miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Kardinali Pengo anasema, kuna kundi kubwa la watoto wanaoendelea kuishi katika mazingira hatarishi si kwa sababu wamependa na kuchagua kuishi huko! La Hasha! Wanalazimika kuishi huko kutokana na ukosefu wa upendo, amani na utulivu kutoka kwa wazazi na walezi wao; hali ngumu ya maisha pamoja na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu hapa duniani. Jamii ijenge upendo wa dhati kwa watoto, vinginevyo, amani na utulivu vinaweza kuwekwa reheani.

Kardinali Polycarp Pengo amewashukuru wafadhili mbali mbali kutoka ndani na nje ya Italia walioamua kuchangia kwanza kabisa katika ujenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi inayoendeshwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na kwa sasa wameamua kuchangia zaidi ili kusikiliza kilio cha watoto waliokuwa wanateseka kutokana na ukosefu wa huduma ya upasuaji na hivyo kulazimika kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu zaidi. Kardinali Pengo anasema, huu ni mfano na kielelezo cha mshikamano wa upendo na wananchi wa Italia.

Huu ni mfano unaopaswa kuigwa na watanzania wengine wote ili waweze kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, tayari kujitosa kimasomaso kuwasaidia kwa hali na mali. Kliniki ya Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi ni mfano hai wa mshikamano wa upendo na maskini na kwa ajili ya mafao ya wengi!

Kardinali Polycarp Pengo amewataka watanzania kujenga moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutunza na kuendeleza kwa ufaanisi na tija miradi mbali mbali inayotolewa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Falsafa ya neno asante ni kuomba tena kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake!

Habari hii imeandaliwa na
Rodirck Minja.
Singida, Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.