Mwenyeheri Yohane Paulo II kutangazwa kuwa Msimamizi wa Siku za Vijana Duniani
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Maadhimisho
ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2014 itakayoadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo,
Jumapili ya Matawi, ambayo kwa Mwaka huu inaadhimishwa hapo tarehe 13 Aprili.
Hii
ni siku ambayo Maaskofu watazungukwa na umati wa vijana kutoka katika majimbo yao
ili kufanya tafakari ya kina kuhusu kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho haya: "Heri
walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao". Hii ni sehemu ya muhtasari
wa mafundisho makuu ya Yesu yanayopatikana katika Heri za Mlimani.
Baraza
la Kipapa la Walei linasema, huu ni ujumbe ambao unatolewa kwa mara ya kwanza kwa
vijana na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Ni mwendelezo wa changamoto ya majiundo endelevu iliyoanzishwa na Mwenyeheri
Yohane Paulo II na kuendelezwa kwa ari kubwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa
kumi na sita.
Papa Francisko bado anakumbuka ule umati wa vijana kutoka sehemu
mbali mbali za dunia uliomzunguka wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013 iliyofanyika mjini Rio de Janeiro. Baba Mtakatifu anaendeleza yale
majadiliano ya kina kati yake na vijana yaliyoibuliwa wakati wa Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani.
Kumbe, ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Kijimbo kwa Mwaka huu, ni sehemu ya maandalizi ya hija ya maisha ya kiroho,
itakayofanyika katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa, kabla ya vijana hawajajimwaga
kuelekea Jimbo kuu la Cracovia, Poland, kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2016.
Wachunguzi wa mambo wanasema, vijana watafunika Poland, ikizingatiwa
kwamba, hizi zitakuwa ni mwendelezo wa utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu
baada ya Mwenyeheri Yohane Paulo II kutangazwa kuwa Mtakatifu. Tema zilizochaguliwa
na Baba Mtakatifu katika kipindi cha miaka mitatu kutoka katika Heri za Mlimani zinazonesha
jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyothamini sehemu hii ya Injili kuwa ni
kiini cha maisha ya Wakristo, mwaliko wa kuyamwilisha katika vipaumbele vyao vya maisha
ya kila siku!
Baba Mtakatifu katika ujumbe kwa Siku ya Vijana Duniani anapenda
kuwakumbusha vijana wa kizazi kipya kwamba, hii ni njia ambayo Yesu mwenyewe amewaonesha
wafuasi wake, mwaliko wa kumfuasa katika maisha yao yote bila ya kujibakiza hata kidogo.
Kumwilisha Heri za Mlimani kwa vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu ni kazi
kweli kweli!
Huu nimwaliko wa kumfuasa Kristo na kushikamana naye kwa dhati,
tayari kutolea ushuhuda wa mabadiliko yanayobubujika kutoka katika undani wa maisha
ya mwamini. Baba Mtakatifu anawachangamotisha vijana kutokubali kupata furaha ya mpito
kwa mambo ya juu juu tu, bali wahakikishe kwamba, wanajitaabisha kutafuta furaha ya
kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu
anafafanua kwa kina na mapana maana ya umaskini wa roho kadiri ya mafundisho ya Yesu,
ambaye aliuchagua mwenyewe na hatimaye kuutolea ushuhuda katika maisha na utume wake
hapa duniani, mwaliko kwa vijana kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Francisko, aliyekuwa
tajiri wa kutupwa, lakini akaacha yote na kuukumbatia ufukara wa Kiinjili. Hii ndiyo
changamoto kubwa iliyoko mbele ya vijana wa kizazi kipya na wala si maji kwa glasi!
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kutubu na kumwongokea Yesu Kristo, huku wakijitahidi
kuishi maisha yanayosimikwa katika kiasi, wakitafuta mambo msingi katika maisha yao
pamoja na kujenga mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Maskini ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo linaloendelea kuteseka, mwaliko
kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaguswa na umaskini, taabu na mahangaiko ya
jirani zake; kwa njia hii vijana wanaweza kuwa kweli ni walimu wa maisha, kwa kuwamegea
wengine utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu unaobubujika kutoka katika undani wa
maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya
tema iliyoongoza Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de
Janeiro "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi..." na kauli mbiu
ya mwaka huu yaani, "Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao".
Ufukara wa Kiinjili ni muhimu sana katika ujenzi wa ufalme wa Mungu sehemu mbali mbali
za dunia. Ni ufukara unaojionesha katika hali ya kawaida pasi na makuu, kiasi cha
kuweza kuwa ni chachu ya Uinjilishaji Mpya.
Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana
wa kizazi kipya kwamba, hapo tarehe 22 Aprili 2014, Kanisa litafanya kumbu kumbu ya
Miaka 30 tangu Msalaba wa Jubilee ya Mwaka wa Ukombozi ulipoanza kutembezwa sehemu
mbali mbali za dunia. Hizi zilikuwa ni juhudi za Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kwa
ajili ya Kanisa, tangu wakati ule, Msalaba umekuwa ni sehemu ya hija ya maisha ya
vijana wa kizazi kipya.
Kwa hakika, baada ya Mwenyeheri Yohane Paulo II kutangazwa
kuwa Mtakatifu, Kanisa litaendelea kumshukuru Mungu kwa kumtangaza rasmi kuwa ni Msimamizi
wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani. Mwenyeheri Yohane Paulo II alikuwa ni muasisi
na mhamasishaji mkuu wa Siku za Vijana Duniani, hadi leo hii, tukio hili linaendelea
kuwa na mvuto na mashiko makubwa katika maisha na utume wa Mama Kanisa miongoni mwa
vijana, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa sasa na kwa
siku za usoni!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.