Makanisa yanapenda kujielekeza katika ujenzi wa misingi ya haki na amani duniani
Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake ulioanza hapo tarehe
7 Februari na unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 12 Februari 2014, pamoja na mambo
mengine unajadili mikakati na utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa kwenye Mkutano mkuu
wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofanyika mjini Busan, Korea ya Kusini
Mwaka 2013. Kamati kuu inapenda kujielekeza zaidi katika hija ya ujenzi wa misingi
ya haki na amani duniani.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni,
walikubaliana kwa pamoja kushirikiana kwa kufanya hija ya pamoja na waamini pamoja
na watu wenye mapenzi mema katika utekelezaji wa maazimio na mikakati iliyoainishwa
wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Dr.
Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema hii ni hija
ya maisha ya kiroho na kiutu, itakayowawezesha waamini kujikita katika ukweli kwa
ajili yao na jirani zao, tayari kujifunua ili kuona utashi wa Mungu unavyowaongoza
katika ulimwengu mamboleo.
Ni changamoto kwa Makanisa kushikamana, ili kufahamu
mambo msingi yanayopaswa kubadilishwa, kwa kuangalia mbinu mkakati na majukumu yatakayojitokeza,
ili waweze kuyatekeleza kwa pamoja! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linataka kuwekeza
zaidi katika misingi ya haki hususan katika maeneo ambamo bado mtutu wa bunduki unaendelea
kusikika hasa nchini: Syria na Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.
Bado kuna pengo kubwa kati ya maskini na matajiri duniani, jambo linalohitaji kujenga
mshikamano wa upendo kwa kuguswa na matatizo ya watu wengine duniani.
Kuna
masuala kama vile: Umoja wa Wakristo, utume wa Makanisa, Ekolojia, Mazingira, misingi
ya uchumi wa haki na haki msingi za binadamu, yanapaswa kuchambuliwa, kufafanuliwa
na kuwekewa mikakati ya utekelezaji wake kwa kutumia Makanisa wanachama!
Baraza
la Makanisa Ulimwenguni linasema, Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: Injili
ya Furaha ni changamoto kwa Baraza hili kushirikiana kwa karibu na Kanisa Katoliki
katika utekelezaji wa mikakati ya kichungaji iliyoainishwa na Papa Francisko katika
dhamana ya utangazaji na ushuhuda wa Injili ya Furaha.