2014-02-08 08:50:43

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu katika kujenga na kudumisha amani na utulivu!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anasema, Jumuiya za waamini pamoja na viongozi wa kidini hawana budi kushikamana kwa pamoja katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu kwa njia ya majadiliano ya kina yanayojengeka katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa niaba ya Makanisa ya Kiorthodox, wakati alipokuwa anahutubia Mkutano wa kumi na saba wa Jumuiya ya Eurasin, uliofanyika hivi karibuni huko Istanbul, Uturuki kwa kuandaliwa na Mfuko wa Marmara. Anasema, kinzani na migogoro ya kijamii ni sehemu ya maisha ya binadamu, wakati mwingine haiwezi kuepukika, lakini binadamu ana uhuru na utashi wa kuzuia na kuepusha majanga ya vita duniani.

Jamii itaendelea kuwakumbuka na kuwaenzi watu mbali mbali wanaojisadaka kwa ajili ya kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, amani na utulivu pamoja na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa kidini na waamini wao kujielekeza katika ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa kudumisha haki na amani duniani.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, historia inaonesha kwamba, chuki na kinzani kati ya Wakristo na Waislam hazina msingi wowote wa kiimani bali zinapata chimbuko lake katika masuala ya kisiasa, kwa baadhi ya wanasiasa kutumia kinzani na misigano ya kidini kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Jamii inapaswa kutambua kwamba, ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia unawahamasisha kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati, kwa kuheshimiana na kuthaminiana, kwani leo hii vikwazo vingi vimepewa ufumbuzi katika utandawazi. Majadiliano ya kidini na kiekumene yanatambua tofauti msingi zilizopo kati ya waamini, lakini pia yanatoa mwanya wa kujadili mambo msingi yanayoweza kuwaunganisha ili kujenga mawasiliano ya dhati katika mchakato wa amani na utulivu.

Ni jukumu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kujikita katika majadiliano yanayopania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanaisho kati ya watu wa mataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.