2014-02-07 07:23:56

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya tano ya Kipindi cha Mwaka wa A wa Kanisa


Tunaendelea na kipindi chetu tafakari Neno la Mungu masomo Dominika ya V ya mwaka A. Masomo yanatualika kuwa chumvi na mwanga wa dunia. Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anatualika kuwalisha na kuwavika maskini. RealAudioMP3
Katika kutenda kazi hiyo tunakumbuka Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao. Kwa njia ya Nabii Isaya, Bwana anatangaza matokeo ya kazi njema hiyo, akisema nuru itakuzukia kama asubuhi na afya yako itakuwa njema na haki daima itakutangulia. Nabii Isaya haishii katika hayo bali pia anatangaza kuwa sala ya mwenye kutenda huduma kwa walio maskini itasikikika daima na hapa ndipo kuna furaha timilifu katika mapenzi yake Mwenyezi Mungu.

Uaguzi wa Nabii Isaya unakuja wakati Waisrael wametoka utumwani Babilonia katika karne ya 5KK. Katika kipindi hicho, Waisraeli walitarajia kuwa mateso yangekuwa yamekwisha, lakini badala yake yaliendelea. Basi kwa kuwa katika nyakati za kale kama kulitokea shida fulani watu walifunga, ni katika mlengo huo basi, Waisraeli walifunga na kusali ili maisha yao yaweze kukaa sawasawa. Pamoja na jambo jema hilo la kufunga shida iliendelea yaani matajiri waliendelea kuwanyonya maskini.

Ni katika madhulumu haya Waisraeli walianza kumlalamikia Mungu, kwa nini mambo hayabadiliki na hivi wakaanza kusema haina haja ya kufunga! Hapa ndipo sasa Nabii Isaya anakuja na jibu akisema Mungu hana kosa lolote, isipokuwa sala na kufunga kwenu hakufikii kiwango cha kumpendeza Mungu. Mungu anataka sala na kufunga kuliko na mzizi katika huduma kwa maskini na wenye taabu mbalimbali katika jumuiya yenu. Mpendwa sala yako ikoje?

Katika Somo la Pili Mt. Paulo anazidi kutangaza nguvu ya Mungu ambayo huongoza wahubiri wa Neno lake. Ndiyo kusema hakuna mhubiri anayeweza kujitapa yakwamba anatangaza injili kwa nguvu zake mwenyewe. Anawaalika Wakorinto watambue kuwa Neno na ujumbe wa Mungu haulali katika ufasaha na hekima ya kibinadamu kama watu wenye hekima katika kizazi hicho cha Wakorinto bali ni nguvu ya Msalaba wa Kristo mfufuka. Yeye mwenyewe anakiri kuwa hakuja kuonesha hekima yake bali kumjua Kristu tu na ndiyo shime yake. Ndiyo kusema anakiri udhaifu wake ambao utamruhusu aombe msaada toka kwa Mungu.

Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 20:9 inaonekana Mt. Paulo alipokuwa anahubiri kuna baadhi walianza hata kusinzia na kijana mmojawapo alianguka kupitia dirishani toka gorofa ya tatu! Ataka kusema nini? Ataka kusema ufasaha hauna nguvu bali Mungu mwenyewe katika Roho Mtakatifu. Na kama ingekuwa ufasaha ni wa maana, basi kijana huyu asingeingia katika shida ya usingizi. Hili halikumtisha Mt. Paulo bali Injili iliendelea kuhubiriwa na kuenea katika Ukorinto yote. Mpendwa unayenisikiliza Neno lenyewe lina nguvu bila madoido yetu, yafaa kuwa na imani thabiti.

Katika Injili ya Matayo, ujumbe na mwaliko ni ”kuweni chumvi na nuru”, na kwa namna hiyo kuangaza mbele ya watu na watu wayaone matendo yenu na wamtukuze Mungu. Mwinjili anatumia mfano wa chumvi na nuru, ambazo ni alama tumika katika nyakati za kale. Chumvi humaanisha mambo kadhaa: chumvi huleta radha kwenye chakula na hivi toka zamani ilimaanisha hekima na busara. Hata hivi leo utasikia watu wakisema, jamaa ana chumvi katika kichwa chake, wakimaanisha ana hekima na busara katika utendaji wake. Ndiyo kusema Wafuasi wa Kristo lazima watoe maneno yaliyo ya maana yaani yaliyojaa hekima ya kimungu na si bulaabulaa!

Jaribu kufikiri kama Neno la Mungu lisingekuwa Neno la furaha wapi tungepata matumaini! Wapi tungepata kutambua kuvumilia taabu na madhulumu katika maisha yetu! Wakristo ni lazima watoe radha ya kikristo ili maisha ya watu yawe ni maisha ya furaha na matumaini.

Mpendwa msikilizaji, chumvi si tu radha bali pia hutumika kutunza vyakula vizioze! Wakristo kwa maana hiyo lazima wawe watunzaji wa maisha ya watu katika ulimwengu huu. Uwepo wa Wakristu katika ulimwengu ni msaada ili mwanadamu asianguke katika unyanganyi na ufisadi na hivi dunia ikaangukia katika kuongozwa na misingi ya shetani.

Mpendwa msikilizaji, kwa kawaida chumvi haipotezi radha yake, sasa iweje Bwana aseme chumvi iliyoharibika? Bwana katika hili ataka kutuambia kuwa kama mhubiri anaacha kumtegemea Mungu na hivi anaweka mambo yake mbele basi ile hali ya Injili uchafuliwa ingawa Injili yenyewe hubaki, lakini kuna uozo huo ambao huchelewesha kasi yake.
Mpendwa mwana tafakari Bwana anatumia mfano wa mwanga akitaka waamini wawe mwanga unaoangaza wengine ili waweze kuona. Kama ambavyo jua huangaza ili tuone vema basi nasi vivyohivyo kwa wengine. Mwanga unao wajibu wa kuangaza kumbe hatuweki macho yetu kwenye mwanga bali kwa kile chema kinachotendwa na mwanga.

Wakristo si mwanga bali wanategemewa kutenda yaliyomema yaani matendo ya mwanga. Wakristo kwa vyovyote vile lazima wabaki wamejificha, kwa sababu ukitazama jua moja kwa moja utaharibu macho, kumbe tunachotakiwa kuona ni hospitali, vituo vya watoto yatima, shule na mambo yote mema yaani matendo ya mwanga. Mpendwa ni kwa njia ya matendo haya Injili ya Bwana inasonga mbele kwa kasi mpaka miisho yote ya dunia.
Nikutakie furaha na matumaini katika kuwa mwanga na chumvi ya dunia. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.