Wanandoa wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kutunziana uaminifu wa viapo vyao
vya ndoa, ili kuhakikisha kwamba, daima ile divai ya upendo, uaminifu, ukarimu, msamaha
na udumifu vinatunzwa na kuendelezwa katika maisha ya ndoa na familia.
Uaminifu
miongoni mwa wanandoa ni tunu msingi katika kukuza na kudumisha malezi ya watoto ambao
ni tumaini la Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Familia zikitekeleza wajibu wake
msingi, Kanisa litaweza kuimarika na kuzaa matunda ya wongofu na utakatifu wa maisha
kwa watoto wake! Wanandoa wanapaswa kuondokana pia na tabia ya kuvunjika kwa ndoa
hata katika uchanga wake hasa kutokana na ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa
na familia.
Hapa kinachoonekana ni upendo wa vitu na mali, mambo ya mpito!
Wanandoa wajenge upendo wa dhati kabisa unaobubujika kutoka katika sakafu ya mioyo
yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Nyumbani. Maisha yao yawe ni utenzi
wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu na harufu nzuri ya matumaini kwa wana ndoa
watarajiwa, ili kwa kuona mifano na ushuhuda amini wa watu wa ndoa, vijana wengi wavutwe
kufunga ndoa za Kikristo; ndoa zinazopaswa kudumu hadi kifo kitakapowatenganisha!
Hii
ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki
Machakos, Kenya wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Upadre
kwa Mashemasi thelathini, kielelezo cha upendo na ukarimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu
unaobubujika kutoka katika Familia za Kikristo. Hawa ni vijana ambao wanataka kujitosa
kimasomaso kuwatangazia watu Injili ya Furaha kwa njia ya maisha na utume wa Kipadre.
Ibada hii ya Misa Takatifu ilikuwa ni sehemu ya Kufunga Mwaka wa Imani uliokuwa umezinduliwa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kufungwa rasmi na Papa Francisko kwa kishindo
kikuu!
Vijana wamechangamotishwa kuwaheshimu, kuwapenda na kuwahudumia wazazi
wao kwani wazazi hawana mbadala duniani! Waamini katika ujumla wao wamehimizwa kuendeleza
hija ya maisha ya kiroho, matunda na neema walizokirimiwa wakati wa Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani.
Katika kipindi cha Miaka kumi iliyopita, Jimbo Katoliki la
Machakos limefanikiwa kupata maendeleo makubwa katika mikakati yake ya shughuli za
kichungaji, jambo la msingi kwa sasa ni kujenga, kuimarisha na kuishuhudia imani yao
katika matendo. Waamini wametakiwa kuwasaidia Mapadre wapya kuishi maisha yao ya Kipadre
kwa uaminifu, uadilifu, uchaji na majitoleo kamili, kama sehemu yao ya kushiriki mchakato
wa kuwatakatifuza watu wa Mungu bila kumezwa na malimwengu.
Askofu Martin Kivuva
ametumia fursa hii kuzindua pia Mwaka 2014 kuwa ni Mwaka wa Familia Jimbo Katoliki
la Machakos. Ibada hii pia ilikuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka
10 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakos baada ya Askofu
Urbanus Kioko aliyelitumikia Jimbo Katoliki Machakos kwa miaka 29 kung'atuka kutoka
madarakani.
Askofu Martin Kivuva tangu alipoteuliwa kuiongoza Familia ya Mungu
Jimbmo Katoliki Machakos, kumekuwepo na maendeleo makubwa: kiroho na kimwili. Idadi
ya Parokia zimeongezeka kutoka Parokia 42 hadi kufikia Parokia 72 kwa sasa. Jimbo
linaendelea kushirikiana na majimbo mbali mbali kutoka Marekani, Ujerumani na Italia
katika kuwatangazia watu Injili ya Furaha.