2014-02-07 08:06:27

Kila mtu anapaswa kupata huduma makini ya afya!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Dawa Kitaifa nchini Italia na katika baadhi ya Nchi za Ulaya inayoadhimishwa hapo tarehe 8 Februari, 2014 anasema, kuna haja kwa Serikali pamoja na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma sawa ya afya, mahali popote pale walipo, lakini maskini, watoto na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii wapewe kipaumbele cha kwanza.

Askofu mkuu Zimowski anasema, katika nchi 90 duniani, takwimu zinaonesha kwamba, ni watu wachache tu ndio wenye uwezo wa kupata huduma ya dawa muhimu katika maisha yao, changamoto ya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano wa kidugu kwa watu wanaoendelea kuteseka kutokana na magonjwa sehemu mbali mbali za dunia kama anavyohimiza Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni wajibu msingi kwa viongozi wa Serikali na watunga sera kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta ya afya.

Askofu mkuu Zimowski anasema, bado watu wengi wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa huduma msingi katika maisha kama vile: chakula, malazi, maji safi na salama, huduma za afya, elimu na mshahara wa kutosha ili kuwawezesha watu kuhudumia familia zao kikamilifu.

Bado kuna umati mkubwa wa wagonjwa wanaoshindwa kupata huduma ya dawa kutokana na hali ngumu ya maisha. Ili kuokoa maisha ya watu, kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo kwa wagonjwa, kwa kuchangia pato ghafi la taifa katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa nchi changa zaidi duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.