2014-02-07 11:36:09

Kampeni ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mashahidi wa Uganda yazinduliwa rasmi!


Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala Uganda, hivi karibuni alizindua Kampeni ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mashahidi wa Uganda inayojulikana kama "Kikungo", itakayofikia kilele chake hapo tarehe 18 Oktoba 2014, wakati Mama Kanisa atakapokuwa anasherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa na Papa Paulo VI kuwa Mashahidi.

Waamini wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanapima kwa kina na mapana maisha yao ya Kikristo mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo zilizotetewa na Mashahidi wa Uganda, kiasi hata cha kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya kifodini.

Mashahidi ni Wakristo waliokumbana na changamoto pamoja na majanga ya maisha, lakini wakawa imara katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Watu wasiogope kukabiliana na changamoto za maisha, bali jambo la msingi ni kusimama kidete katika misingi ya imani na maadili.

Waamini wametakiwa kukua katika Imani wanayoiungama katika Kanuni ya Imani; imani wanayoiadhimisha kwa njia ya Sakramenti Saba za Kanisa; Imani wanayoimwilisha katika maisha kwa kuongozwa na Amri za Mungu pamoja na Kanuni msingi za kimaadili na utu wema; hii ndiyo imani wanayopaswa kuisali kwa kufuata Zaburi na ile Sala kuu ya Baba Yetu wa Mbinguni. Waamini wasikubali kuyumbishwa kwa njia ya imani za kishirikina zinazoendelea kuwatumbikiza katika utupu na umaskini wa hali na kipato.

Fedha wanazotoa kwa ajili ya kuwapatia waganga wazitumie kwa ajili ya maendeleo endelevu. Askofu mkuu Lwanga katika Ibada ya Kuzindua Mwaka wa Mashahidi wa Uganda, alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa Watoto 40 na Wanandoa 25 walifunga ndoa zao ndani ya Kanisa, tayari kuanza mchakto wa ujenzi wa Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa: utakatifu wa maisha, sala na ukarimu kwa Mungu na jirani.







All the contents on this site are copyrighted ©.