Maaskofu wanashirikishana Injili ya Furaha pamoja na kuangalia mbinu mkakati wa kudumisha
haki na amani duniani!
Maaskofu kutoka Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Ulaya, ni kati ya mahujaji waliokuwa
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano tarehe 5 Februari
2014, kusikiliza kwa makini Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu umuhimu wa
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu hawa wako
mjini Roma ili kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 46 tangu Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio yenye makao makuu yake mjini Roma ilipoanzishwa.
Mkutano huu wa kumi
na sita unaongozwa na kauli mbiu "Injili ya Furaha", tema inayotoa mwanya kwa Maaskofu
kubadilishana uzoefu, mang'amuzi na vipaumbele vyao katika mchakato wa kuwatangazia
watu Injili ya Furaha ili kuwajengea matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo
na Kanisa lake.
Maaskofu hawa wanatumia fursa hii kushirikishana uzoefu na
mang'amuzi yao katika: kutakatifuza, kufundisha na kuwaongoza watu wa Mungu. Mama
Kanisa anaendelea kuwahamasisha Maaskofu kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baadhi ya Maaskofu ni wale wanaotoka
katika maeneo ambayo yameguswa kwa namna ya pekee na mashambulizi ya kigaidi, vita
na kinzani za kijamii na kisiasa kama vile: Nigeria, DRC, Uganda, Syria na maeneo
mengine ambako bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika.
Maaskofu
katika mkutano huu ulioandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio wanajadili pamoja na
mambo mengine umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani
na udugu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatafuta mbinu mkakati wa kutatua vita na
migogoro inayoendelea kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia.
Mkutano huu
unawajumuisha pia Maaskofu kutoka Kanisa la Kiorthodox na Kianglikani. Katika hotuba
yake ya ufunguzi, siku ya Jumatano tarehe 5 Februari, 2014 Professa Andrea Riccardi
amezungumzia kuhusu changamoto za kichungaji zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu
Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.
Alhamisi tarehe 6 Februari 2014,
Maaskofu watahudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane
wa Laterano kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 46 tangu Jumuiya ya Mtakatifu Egidio
ilipoanzishwa. Maaskofu pia wamepata nafasi ya kutembelea Makatacombe ya Ardeatine
yaliyoko mjini Roma.