2014-02-05 07:45:38

Kliniki ya Upasuaji wa Watoto Katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, kufunguliwa rasmi na Kardinal Pengo!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, hapo tarehe 7 Februari 2014 anatarajia kufungua Kliniki ya Upasuaji wa Watoto Wadogo katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida, Tanzania. RealAudioMP3

Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa pia na Professa Giuseppe Profit, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican mjini Roma pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Serikali ya Tanzania.

Kliniki ya Upasuaji kwa Watoto kutoka Kanda ya Kati nchini Tanzania ni kielelezo cha ushirikiano wa huduma ya upendo na mshikamano kati ya Hospitali ya Bambino Gesù na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar Itigi inayoendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu.

Katika mahojiano maalum na Padre Seraphine Lesiriam, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, anabainisha kwamba, Kliniki hii imeanzishwa ili kukabiliana na changamoto za magonjwa mbali mbali yanayowakabili watoto hususan kutoka Kanda ya Kati nchini Tanzania; magonjwa ambayo yanahitaji matibabu maalum pamoja na kupunguza gharama za matibabu kwa watoto ambao walikuwa wanalazimika kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

Tangu Mwaka 2005 Hospitali ya bambino Gesù ilianzisha uhusiano wa tiba na Hospitali ya Mtakatifu Gaspar kwa ajili ya kuwasaidia watoto waliokuwa na magonjwa ya moyo. Kuanzia mwaka 2006 hadi kufikia Mwaka 2012 jumla ya watoto 13 wamenufaika na huduma ya upasuaji wa moyo iliyokuwa inatolewa na Hospitali ya Bambino Gesù. Mtoto mmoja amepewa huduma ya marekebisho ya ngozi. Kwa bahati mbaya katika kipindi hiki, mtoto mmoja alifariki dunia, hali yake ilikuwa mbaya tangu alipowasili nchini Italia kwa ajili ya kufanyiwa Operesheni ya moyo.

Padre Serafini anasema, Hispitali ya Bambino Gesù imechangia kiasi cha Euro 250, 000; sawa na shilingi za kitanzania Millioni 525 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo yatakayotumiwa na Kliniki ya Upasuaji kwa ajili ya Watoto, Hospitali ya Mtakatifu Gaspar. Lengo ni kuwa na uhakika wa huduma za kibingwa za upasuaji kwa ajili ya watoto badala ya kulazimika kuwasafirisha kwenda Italia kwa matibabu zaidi, kama ilivyokuwa hapo awali.

Hopistali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar kwa sasa imekamilisha huduma za tiba zifuatazo kwa ajili ya watoto wagonjwa: Upasuaji wa moyo; meno na macho; huduma ya tiba kwa njia ya mtandao, yaani “tele-medicine”. Idara ya wagonjwa mahututi pamoja na kitengo cha elimu na burudani kwa watoto wanaolazwa Hospitalini.

Hospitali ya Mtakatifu Gaspar ilizinduliwa rasmi hapo tarehe 15 Mei 1989 na Rais wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi. Tarehe 12 Oktoba 2010 ikapandishwa hadhi na kuwa ni Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa. Kwa sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 320 kwa wakati mmoja.

Takwimu zinaonesha kwamba, Idadi ya wagonjwa waliohudumiwa Hospitalini hapo katika kipindi cha Mwaka 2013ni wagonjwa wa nje chini ya umri wa miaka mitano walikuwa ni 9, 404 na wagonjwa wa nje wenye umri zaidi ya miaka 5 walikuwa ni 36, 353. Wagonjwa waliolazwa na kupatiwa huduma Hospitalini hapo walikuwa ni 8, 133, kati yao wagonjwa 3, 711 walikuwa ni watoto wadogo. Ndiyo maana Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar inaendelea kuwekeza katika huduma kwa watoto ili kupunguza vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka 5 mintarafu mpango mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa.

Padre Serafini anaendelea kubainisha kwamba, ili kuendeleza mchakato wa maboresho ya huduma ya afya kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, kunako tarehe 4 Septemba 2006, Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspar, kilianzishwa. Chuo kinatoa stashahada na cheti ili kukidhi mahitaji ya rasilimali watu katika sekta ya afya nchini Tanzania.

Padre Serafini anasema, zote hizi ni juhudi za Uinjilishaji wa kina unaofanywa na Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ili kujibu kilio cha damu kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Shirika linaendelea kutoa huduma katika sekta ya elimu na mradi wa maji safi na salama kwa ajili ya mikoa iliyoko Kanda ya kati, nchini Tanzania. Shirika limekuwa ni mdau mkuu wa maendeleo endelevu Kanda ya kati.

Padre Serafini Lesiriam, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi anasema, Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika huduma za kiushauri, rasilimali watu, dawa na vifaa. Mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya Hospitali ya Rufaa Bugando, inayomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii, CSSC bila kuwasahau AMREF.

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar inakabiliana pia na changamoto kubwa kama vile: upungufu wa rasilimali watu na fedha kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa ruzuku iliyokuwa inatolewa na wafadhili kutoka ndani na nje ya Tanzania kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ongezeko kubwa la gharama za dawa na vifaa tiba pamoja na upatikanaji wake kwa wakati muafaka.

Itakumbukwa kwamba, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar iko Kanda ya Kati, nchini Tanzania, eneo ambalo halina nguvu kubwa ya kiuchumi, kumbe, sehemu kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa Hospitalini hapo hawana uwezo mkubwa kiuchumi. Wananchi wengi bado hawana mwamko wa kupata elimu ya kukinga na kutibu magonjwa, kiasi kwamba, wanalazimika kwenda Hospitalini pale wanapokuwa wamezidiwa sana!

Habari hii imeandaliwa na
Rodrick Minja kutoka Radio Mwangaza, Dodoma
na kuhaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.