Walengwa washirikishwe kikamilifu katika Jukwaa la Ardhi Tanzania
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Jukwaa la Ardhi linapaswa kushirikisha
walengwa katika ngazi zote ili liweze kufanikiwa kuisaidia Serikali katika kutatua
migogoro ya ardhi. “Amani ni tunu ya pekee ambayo kila mmoja wetu hana budi kuidumisha
na kuipa uzito ili kuleta maendeleo ya Taifa letu. Ametoa kauli hiyo wakati akizindua
Jukwaa la ardhi Tanzania Jumanne, Februari 04, 2014 katika Ukumbi wa Golden Jubilee
Towers jijini Dar es Salaam. “Pasipo amani, utulivu wa kufanya kazi iwe ni kilimo
ama ufugaji hautapatikana na hivyo maendeleo ya mtu, kikundi cha watu ama Taifa yatabaki
kuwa ndoto isiyoweza kutimia,” alisema. Alisema kuzinduliwa kwa Jukwaa hili ni
njia mojawapo itakayosaidia katika kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa na viashiria
vya kupotea kwa amani ya Taifa: “Badala ya Ardhi kuwa msingi wa amani, na chanzo kikuu
cha maendeleo na uzalishaji, inaanza kutugawa na kutuleea migogoro ya mara kwa mara”. “Mtazamo
wa Serikali kwa chombo hiki ni kwamba kitaleta na kukutanisha wadau mbalimbali ili
kupeana uzoefu na kushirikishana na baadaye kuona mambo ya migogoro ya ardhi yanakuwa
historia katika nchi yetu nina imani mtafanikisha”, alisema. Ameagiza Jukwaa lijipange
kujitegemea na kujitoa kufanyakazi kwani katika utekelezaji wa maazimio hayo lazima
watakutana na changamoto nyingi sana, hivyo washirikishe jamii katika kila hatua ili
kuweza kutekeleza maazimio yao: ”Kila mmoja atoke na dhamira kwamba tulichokizindua
leo hakina msamiati wa kushindwa”. “Jukwaa hili liwe chanzo cha elimu yenye tija
itakayowezesha wanajamii kuiona na kuitumia ardhi yao huku wakizingatia sheria na
kutumia zaidi tafiti mbalimbali,mipango na mikakati ya kimaendeleo kuhusisiana na
ardhi”, alisema Waziri Mkuu. Viongozi wa Dini mna nguvu ya kipekee kwani wananchi
wana imani kubwa nanyi hivyo tumieni imani hiyo vizuri ili muweze kutatua migogoro
ndani ya Jukwaa hili”, alisisitiza. Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau
walioshiriki uzinduzi huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT),
Dkt. Alex Malasusa alisema ardhi aliyoumba Mungu, haiongezeki bali wanadamu wanaongezeka
na kama watu hawana mipango mizuri ya ardhi ni lazima patokee migogoro. “Usimamizi
mzuri utazuia migogoro na kuepuka gharama zisizo za lazima. Tuko tayari kutoa mchango
wetu kupitia Jukwaa la Ardhi la Tanzania ili wananchi wapate nafasi ya kushirikishwa
kwa ukaribu zaidi”. Mapema, akiongea katika uzinduzi huo Askofu Dk. Steven Munga
amesema Jukwaa hili limeanzishwa ili kuelimisha na kuhabarisha jamii kwa njia ya ushirikishwaji
wa taarifa kupitia jukwaa mbalimbali ambayo itasaidia watu kupata uelewa wa ukweli
utaopunguza migogoro ya Ardhi. Alisisitiza kuwa Jukwaa la Ardhi litatumia dhana ya
ushirikishwaji katika kujadili mambo yamayowahusu watu, na tunaamini kuwa ndio dhana
bora ya Uongozi. “Nia ya Jukwaa ni kutoa nafasi kwa watu kutoa mawazo yao na kuayafanyiakazi
kwa kushirikishwa”.