Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 13 Februari 2014 itaadhimisha Siku ya Radio Duniani
inayokazia Radio kama chombo muhimu sana katika mawasiliano ya kijamii, changamoto
kwa wadau mbali mbali kushirikiana kwa karibu zaidi pamoja na kuendelea kuhamasisha
matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kutoa habari, kukuza na kuendeleza uhuru
wa mtu kujieleza. Ni fursa ya kukuza na kuimarisha usawa na umoja kati ya watu!
Radio
bado inaendelea kufanya kazi zake msingi hata katika maendeleo ya teknolojia ya digitali,
jambo ambalo linaviwezesha vituo vingi vya Radio kuweza kuufikia umati mkubwa wa watu
sehemu mbali mbali za dunia. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa,
UNESCO, linasema, kuna haja kwa Radio kusaidia kampeni ya Umoja wa Mataifa katika
kujenga na kudumisha usawa kati ya watu pamoja na kuimarisha mchango wa wanawake ndani
ya Jamii.
Huu ni mchango unaoweza kutekelezwa na waandishi wa habari kwa kukazia
usawa kati ya mwanaume na mwanamke katika utekelezaji wa majukumu yao. Kuna haja kwa
wadau mbali mbali kuwa na matumizi makubwa zaidi ya mitandao ya kijamii pamoja na
kusaidia kulinda na kutetea usalama wa waandishi wa habari wanawake wanaotekeleza
jukumu lao katika Vituo vya Radio sehemu mbali mbali za dunia.