Malkia Elizabeth wa Uingereza kukutana na Papa Francisko tarehe 3 Aprili 2014
Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 3 Aprili 2014 anatarajiwa kukutana na kuzungumza
na Malkia Elizabeth wa Uingereza pamoja na ujumbe wake, ambao watakuwa mjini Roma
kwa mwaliko wa Rais Giorgio Napolitano wa Italia. Malkia Elizabeth amealikwa na Serikali
ya Italia kwa chakula cha mchana na baadaye atapata fursa ya kukutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Francisko.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Malkia Elizabeth
kukutana na Baba Mtakatifu Francisko aliyechaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki hapo
tarehe 19 Machi 2013, baada ya Papa Benedikto XVI kung'atuka kutoka madarakani kwa
hiyari yake mwenyewe. Kwa mara ya mwisho, Malkia Elizabeth wa Uingereza alitembelea
mjini Roma tarehe 17 Oktoba 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Ukristo,
akakutana na kuzungumza na Mwenyeheri Yohane Paulo II.
Malkia Elibeth alikutana
na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mwezi Septemba, 2010 wakati alipokuwa anatembelea
Uingereza. Itakumbukwa kwamba, Malkia Elizabeth aliwahi kukutana na Papa Yohane XXIII
kunako mwaka 1961. Habari hizi zimethibitishwa na Padre Federico Lombardi, msemaji
mkuu wa Vatican.