2014-02-03 08:16:47

Wapeni wanandoa nafasi ya kujinafasi! Msiwawekee kiwingu!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, Kipindi cha Kanisa la Nyumbani kilichopita, tumehekimishana juu ushiriki wa Jamii katika kuifanya ndoa ianze vyema na kustawi. RealAudioMP3

Tuliangazia kwanza wajibu wetu wa kuwaombea wanandoa ili waweze kustawi kama mtende wa Lebanoni na pili, tunatakiwa kuwapatia ushuri mwema, kila mmoja wetu akijitahidi kuwa na ”kifua kipana”, yaani kubeba na kutunza siri za wanandoa. Leo tunaendelea na sehemu ya tatu!

Tatu, TUWAPE NAFASI:- Watu wa ndoa, hasa ndoa changa, wanahitaji muda wa kufahamiana zaidi, kuendelea kukua, kujijenga, kufurahiana wao wenyewe nk. Hapa tutoe mwito pia kwa baadhi ya ndugu. KUWENI NA MIPAKA, tena iweni na aibu takatifu. Tabia ya ndugu kwenda kujazana nyumbani kwa waana waliotoka tu kuoana, ni kuwabana mno.

Utashangaa ukoo mzima wa Bibi harusi wamejaa tele hapo, wameleta matatizo yao yote. Ukoo wa Bwana harusi wamejaa humo, na ni wakorofi, walafi na wapekuzi ajabu. Mwisho wanaishia kuwachonganisha wanandoa-changa. Bandika – bandua, akitoka huyu, anakuja huyu. Ndugu wawe na mipaka, ndoa ya mtoto wenu sio sokoni. Wanahitaji faragha hao.

Nne, KUTAWALA MIDOMO YETU: Katika hili, mang’amuzi yatatushuhudia kwamba, mara nyingi sana jamii tumechangia kuyumbisha ndoa za watu kwa kukosa matumizi ya busara ya midomo yetu. Kanuni moja inatuelekeza hivi: Sio kila unachokijua lazima ikiseme! Vingine kaa navyo kimya tu - ufe navyo, wala jeneza halitakuwa zito!! Sasa ewe mtu, kuna mambo unayajua kuhusu mke wa fulani au mume wa fulani.

Usikurupuke tu na kuanza kutangaza au kwenda kumwambia mama fulani habari-hatarishi unazozijua za mumewe; au unamwambia baba habari hatarishi za mkewe. Na unapokwenda kumwambia, humwambii habari kama ilivyo, lazima utatia chumvi nyingi na pilipili yenye kuwasha, ambayo lazima itawachachafya na kutikisa safari yao ya agano tu; na wakitikisika, wewe unafurahi!! Hapana!! Kama ni lazima sana, ukiona mama fulani anafanya kinyume – nenda kamwambie yeye mwenyewe, tena umkanye kabisa.

Sio umamchekea tena na kumsaidia katika uovu, halafu unamzunguaka na kwenda kumripoti kwa mumewe. Ukiona baba fulani anafanya visivyo; MWAMBIE YEYE MWENYEWE, UMKANYE, usipitilize tu kwenda kumpelekea BP mkewe. [Kwa habari ya uchongezi na uchonganishi; soma kwa kutafakari YbS, 28:13 – 26]

Tano na Mwisho: TUTAKIANE MEMA. Roho mbaya zinazojengeka katika mioyo ya watu, ni sumu kwa usitawi wa ndoa na Kanisa la Nyumbani. Kuna watu ni waharibifu tu, wanapenda wenzao waharibikiwe. Kama tulivyokwisha kusema hapo juu, ni wajibu wetu sisi sote kusaidiana katika kulijenga Kanisa la Nyumbani, hatutatimiza adhma hiyo kama hatutakiani mema.

Tujijengee dhamiri iliyo njema, yenye kupenda na kufurahia usitawi wa wengine pia. Kama wewe una roho mbaya, hupendi mafanikio ya wenzako; na wakifanikiwa wewe unaharibu; halafu wakati huohuo, unamwomba Mungu akusaidie ufanikiwe; unadhani sala yako itapata kibali kweli? Mwenyewe katika Neno lake ametukataza, usimtendee mwenzako lile usilopenda kutendewa. Kumtakia mema mwenzako na kumsaidia mwenzako ili kuyapata yaliyo mema, ni kujibariki mwenyewe na kujifungulia milango ya baraka zaidi.

Katika kipindi kijacho tutaanzazia mambo ya jumla ambayo yanaweza kuathiri utimilifu wa Agano la ndoa tangu mwanzoni; YAANI VIZUIZI VYA NDOA, kadiri ya sheria ya Kanisa. Asanteni kwa kuwa nami, kutoka katika Studio za Radio Vatican, kukuletea kipindi cha Kanisa la Nyumbani ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.