2014-02-03 09:34:55

Senegal hapatoshi! Vijana 25, 000 kutinga Jimboni Kaolack


Zaidi ya vijana 25, 000 wanatarajiwa kushiriki katika Siku ya Vijana Kikanda, itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 9 Februari 2014, kwenye Jimbo Katoliki la Kaolack, Senegal. Maadhimisho haya yanapania kuwaonjesha vijana kutoka Barani Afrika uzoefu na mang'amuzi ya Siku za Vijana Kimataifa. Hiki kitakuwa ni kipindi cha majiundo ya imani, utume na changamoto ya toba na wongofu wa ndani.

Vijana wanaalikwa kushuhudia furaha ya kuwa ni Mkristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao pamoja na kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Vijana watawashirikisha wenzao furaha ya kuwa Mkristo na kwamba, kama Jumuiya ya Waamini wanatumwa kwenda sehemu mbali mbali za dunia kuwaonjesha jirani zao ile Injili ya Furaha na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu hakuna mtu anayebaguliwa!

Akizungumzia kuhusu tukio hili, Askofu Benjamin Ndiaye wa Jimbo Katoliki Kaolack anabaianisha kwamba, huu ni muda muafaka kwa Vijana kutoka Barani Afrika kukutana kwa pamoja, ili kutafakari Neno la Mungu na kusali pamoja. Kardinali Thèodore Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal atafunga maadhimisho haya kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa hapo tarehe 9 Februari, kwenye Uwanja wa Michezo wa Lamine Gueye.

Lengo la Ibada hii ni kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya Familia ya Mungu Barani Afrika inayowalilia watoto wake wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita, kinzani na majanga. Ni watoto wa Afrika wanaoteseka kwa kunyanyaswa n akudhuliwa kutokana na kulazimika kuzikimbia nchi na makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Vijana watamegewa kuhusu mambo yanayoendelea kulizunguka Bara la Afrika. Ibada hii inapania pamoja na mambo mengine, kuwatangazia Vijana Barani Afrika Injili ya Kristo; kuwawezesha vijana kuyafahamu Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa, ili hatimaye, waweze kuyatolea ushuhuda wa furaha ya imani, tayari kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza Injili ya Furaha, wakitambua kwamba, wao ni mahujaji wa imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.