2014-02-03 10:49:18

Changamoto kwa vyombo vya habari Barani Afrika kuelekea kwenye mfumo wa digitali!


Wajumbe wa Shirikisho la Watangazaji Barani Afrika, AUB, wamehitimisha mkutano wake wa Saba uliofanyika mjini Yaounde, Cameroon kwa kuwachagua viongozi wakuu pamoja na kukazia umuhimu wa vyombo vya habari Barani Afrika kusimama kidete kulinda na kutetea haki na amani pamoja na kupata leseni zitakazowawezesha kurusha matangazo ya michezo ya kimataifa, matukio muhimu kwa wananchi wengi Barani Afrika.

Watangazaji Barani Afrika hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika ubora wa matangazo pamoja na kwenda na mabadiliko ya teknolojia ya habari duniani, hasa wakati huu mfumo wa habari unapoendelea kuogelea katika masuala ya digitali. Wajumbe wamehimizwa kudumisha umoja na ushirikiano ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu wa habari na mawasiliano.

Baada ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Watangazaji Barani Afrika, wajumbe walitoa tamko linaloonesha ugumu kwa baadhi ya nchi kubadili mfumo wa matangazo yake kutoka analogia kwenda katika mfumo wa digitali. Inawezekana kwamba, nchi nyingi za Kiafrika haziwezi kufikia lengo la kuhamia kwenye mfumo wa digitali ifikapo tarehe 17 Juni 2015.

Wanaliomba Shirikisho la Njia za Mawasiliano Kimataifa kuziangalia nchi za Kiafrika kwa upendeleo maalum pamoja na kuzipatia njia mbadala ili ziweze kuendelea kurusha matangazo yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.