Vinana na wazee wanakutana; wanaongozwa na Roho Mtakatifu kutekeza sheria na unabii!
Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni ni kielelezo ambacho kwa mara ya kwanza Yesu anakutana
na watu wake; ni mkutano kati ya vijana yaani Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wakiwa
na Mtoto wao Yesu Kristo na wazee wanaowakilishwa na Mzee Simeoni na Anna, waliokuwa
Hekaluni. Ni Siku ya 18 ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili kunako mwaka 1997.
Watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume
wamekusanyika, Siku ya Jumapili tarehe 2 Februari 2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican ili kuungana na Baba Mtakatifu Francisko aliyeadhimisha Ibada
ya Misa hii kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika
mahubiri yake anasema, Wazazi wa Yesu walitaka kutekeleza kwa furaha kile kilichokuwa
kimeandikwa katika Sheria ya Mungu, kwani walitambua kwamba, furaha ya kweli inabubujika
kutoka katika Amri za Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, Mzee Simeoni na Anna:
wachamungu na watu wa haki waliongozwa na Roho Mtakatifu, huku wakiwa wamesheheni
maisha, wakakutana Hekaluni. Ni mkutano ambao unawaonesha vijana wakiwa wamejaa furaha
katika kutekeleza Sheria ya Mungu na wazee wakiwa wanafurahia kazi ya Roho Mtakatifu.
Kwa pamoja wanakutana katika kutekeleza sheria na unabii. Vijana katika tukio yaani
Maria na Yosefu wanatekeleza sheria na Wazee wanatimiza Unabii.
Hii inaonesha
kwamba utekelezaji wa sheria ni kazi na hamasa kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba,
Unabii unatekelezeka kwa kufuata mkondo wa sheria. Bikira Maria alikuwa amejaa nguvu
ya Roho Mtakatifu na mnyenyekevu kwa Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu anasema,
huu ndio mwanga ambao Mama Kanisa anapenda kuuangalia mintarafu maisha ya kuwekwa
wakfu ndani ya Kanisa. Huu ni mkutano kati ya Watawa na Kristo. Yesu anakuja kuwatembelea
watu wake, akiwa amebebwa na Bikira Maria Mtakatifu Yosefu, changamoto kwa watawa
na waamini katika ujumla wao, kumwendea ili waweze kukutana naye, huku wakiwa wameongozwa
na nguvu ya Roho Mtakatifu.
Waamini wanakumbushwa kwamba, kiini cha mkutano
huu ni Yesu mwenyewe, anayeongoza na kuwavuta watu kumwendea Hekaluni, Kanisani na
mahali popote ambapo, waamini wanaweza kukutana, kumtambua, kumpokea na kumkumbatia
Yesu.
Baba Mtakatifu anawaambia Watawa kwamba, Yesu anakutana nao ndani ya
Kanisa kwa njia ya karama za waanzilishi wa Mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume
na huu ndio mwanzo wa maisha na wito wao wa kitawa. Maisha haya yanamwilishwa ndani
ya Kanisa kwa njia ya karama iliyotolewa ushuhuda na mwanzilishi wa Shirika, hili
ni jambo linaloshangaza na mwaliko wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani.
Baba
Mtakatifu anasema kwamba, katika maisha ya kitawa kuna mwingiliano kati ya wazee na
vijana; kiini cha utekelezaji wa sheria na unabii. Mambo haya mawili ni sawa na chanda
na pete na wala hakuna ukinzani wowote. Ni mwaliko kwa watawa kumwachia nafasi Roho
Mtakatifu ili awasaidie kutekeleza majukumu haya mawili kwa ufanisi mkubwa, katika
furaha ya kutekeleza na kumwilisha sheria ya maisha. Ni furaha ya mtu anayeongozwa
na Roho Mtakatifu; bila ya kuwa na moyo mgumu wala kujifungia katika ubinafsi wake,
bali mkweli na muwazi katika kuisikiliza sauti ya Mungu inayozungumza naye; ni Mungu
anayefungua na kuelekeza.
Baba Mtakatifu anawaalika wazee kuhakikisha kwamba,
wanajitahidi kuwashirikisha na kuwamegea vijana hekima na busara; vijana nao wawe
tayari kupokea na kumwilisha hazina hii kubwa ya uzoefu na hekima ili kuweza kuiendeleza
mbele kwa ajili ya mafao na ustawi wa Mashirika ya Kitawa na Kanisa katika ujumla
wake. Baba Mtakatifu mwishoni mwa mahubiri yake awaombea wote akisema, neema ya Fumbo
hili la kukutana, liwe ni mwanga na faraja katika hija ya maisha yao ya kiroho!
Itakumbukwa
kwamba, Ibada hii ya Misa Takatifu ilianza kwa Maandamano ya Watawa waliokuwa wamebeba
mishumaa, alama ya Kristo Mwanga wa Mataifa anayeingia Hekaluni, yaani nyumbani mwa
Baba yake.