2014-02-02 09:40:15

Ili kudhibiti Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kuna haja ya kuwa na uelewa mpana zaidi! Mtutu wa bunduki haujafua dafu hadi sasa!


Kardinali John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria hivi karibuni alisema kwamba, tatizo la mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram nchini NIgeria yanapaswa kuangalia kwa kina na mapana badala ya Serikali kuwekeza zaidi katika kupambana nao kwa njia ya mtutu wa bunduki.

Hadi sasa Serikali ya Nigeria imetumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kupambana na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haramu lakini bado watu wanaendelea kupoteza maisha na mali zao kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Tatizo la Boko Haram linapaswa kuangaliwa katika msingi ya: kijamii, kisiasa, kiuchumi na kisaikolojia, ili kubaini ni jambo gani ambalo linawasukuma baadhi ya watu hata baada ya kuelimishwa na kufaulu vyema katika masomo yao ya Chuo kikuu, bado wanadiriki kukimbilia msituni ili kuendesha vitendo vya kigaidi. Kardinali Onaiyekan anasema, hapa kuna tatizo!

Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram yana uhusiano mkubwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani, jambo ambalo kamwe halimwezi kupuuziwa, changamoto ya kuangalia pia mchango wa dini katika kuhamasisha waamini wake kuwa na misimamo mikali kiasi hata cha kusababisha mauaji makubwa kwa jina la Mwenyezi Mungu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha mafundisho na misimamo ya kidini.

Hapa kuna haja kwa viongozi wa Serikali na dini mbali mbali nchini Nigeria kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyosababishwa na Boko Haram nchini Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.