2014-02-01 16:13:55

Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 18 ya Watawa Duniani


Kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na siku 18 ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Hii ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa na kama sehemu ya mchakato wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Ni siku ambayo Mama Kanisa anapenda kuwapongeza watawa kwa ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya mashauri ya Kiinjili pamoja na kurudia tena mambo msingi yaliyowavuta watawa kuacha yote kwa ajili ya kutangaza Injili ya Furaha. Watawa ni watu walioacha yote kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu hapa duniani. Watawa wanajitahidi kumuiga na kumfuasa Yesu Kristo aliyetolewa Hekaluni, changamoto kwa watawa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linafafanua kwamba: kuna Mashirika ya Kitawa ambayo kadiri ya sheria na kanuni za maisha yao watawa wake wanaweka nadhiri na kuishi katika maisha ya kijumuiya. Ni Watawa wanaoalikwa kumwiga Kristo kwa njia ya ushuhuda wa Mashauri ya Kiinjili pamoja na tafakari ya kina ya Neno la Mungu.

Kuna Mashirika ya Kitawa kwa ajili ya walei, wanaojiweka wakfu kwa ajili ya kutangaza Ufalme wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mara ya kwanza Mashirika haya yalitambuliwa rasmi na Mama Kanisa kunako mwaka 1947 na kufafanuliwa kwa kina na mapana katika Sheria za Kanisa za Mwaka 1983. Hawa ni watawa wanaoishi maisha ya kawaida, wakijitahidi kujibu wito kutoka kwa Kristo na kumwilisha ndani mwao Mashauri ya Kiinjili. Yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili katika moyo wa Kheri za Mlimani.

Haya ni mashirika ya kitawa yanayojitahidi kumwilisha mwaliko wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa wote.

Mashirika ya Kazi za Kitume: Haya ni Mashirika ambayo watawa wake hawaweki nadhiri, lakini utume wao unajikita katika maisha ya kijumuiya wakishikamanishwa na kifungo cha upendo kwa kuishi kikamilifu Sheria na Kanuni za Shirika husika.

Mashirika ya Watawa binafsi: Hili ni kundi la Mabikira wanaojiweka wakfu kwa ajili ya Kanisa, hawalazimishwi kuishi maisha ya kijumuiya, bali wanajitahidi kuishi kama waamini walei. Hawa ni kama kile kikundi cha wanawake wanaosimuliwa kwenye Agano Jipya, waliokuwa wanamfuasa Yesu.

Aina hii ya watawa imeibuka kwa nguvu zaidi baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa waamini kujiweka wakfu kwa kutaka kushuhudia fadhila ya usafi kamili katika Ibada inayofanywa na Askofu mahalia. Wito na utume wao ni kubaki ulimwenguni ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya huduma mbali mbali wanazotenda!







All the contents on this site are copyrighted ©.