2014-02-01 08:19:16

Mwaka wa Watawa Duniani 2015 na Malengo yake Makuu!


Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Ijumaa tarehe 31 Januari 2014 amepembua kwa kina na mapana Malengo makuu ya Maadhimisho wa Mwaka wa Watawa Duniani, utakaoadhimishwa Mwaka 2015. Anasema, hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume mjini Vatican, tarehe 29 Novemba 2013.

Huu ulikuwa ni mkutano wa kirafiki kati ya Baba Mtakatifu na Wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume. Baba Mtakatifu aliulizwa maswali kadhaa na kuyapatia majibu, akitumia uzoefu na mang'amuzi yake kama mtawa na kiongozi wa Kanisa. Changamoto hii imefanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, linaoonesha matumaini makubwa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, katika mchakato wa kukoleza ari na moyo wa maisha na utume wa kitawa ndani ya Kanisa.

Lengo la kwanza anasema Kardinali Joao Braz de Aviz ni kwamba, Mwaka wa Watawa unatarajiwa kuwa ni kipindi cha neema na baraka kwa watawa na Kanisa katika ujumla wake. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Jubilee ya Miaka 50 tangu Hati kuhusu Mapendo Kanili, yaani Perfectae Caritatis, ilipotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kina katika maisha na utume wa watawa: kwa kusoma alama za nyakati, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuwa waaminifu kwa karama za mashirika yao pamoja na kumwangalia mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Miaka 50 tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kimekuwa ni kipindi cha neema na baaraka kutokana na uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kimekuwa ni kipindi ambacho kimeonesha udhaifu wa maisha ya watawa kwa kutokuwa waaminifu kwa Mashauri ya Kiinjili na Karama za Mashirika yao, changamoto ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu. Mwaka wa Watawa unapania kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya maisha ya kitawa, kwa miaka iliyopita na kwa sasa.

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume aliwakumbusha kwamba, Kanisa linatambua uwepo wa neema ya Mungu katika maisha na utume wake pamoja na kukiri kwamba, bado kuna dhambi ambazo zinawaandama watoto wake katika hija ya maisha yao!

Mwaka wa Watawa ni kutambua kwa unyenyekevu mkubwa mapungufu yanayojitokeza katika maisha ya kitawa, lakini pia kupaaza sauti kwa nguvu na furaha kwa utakatifu na uhai wa maisha ya kitawa katika utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wanajitahidi kumwonesha Mwenyezi Mungu ambaye ni Mtakatifu sana katika ubinadamu, licha ya uwepo wa dhambi, lakini bado neema ya Mungu inaendelea kutenda kazi!

Kardinali Joao Braz de Avis anasema, Lengo la Pili la Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni kuwa na matumaini kwa siku za usoni kwa kutambua changamoto na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa watawa sehemu mbali mbali za dunia, kama ambavyo aliwahi kudokeza Mwenyeheri Yohane Paulo II. Mmong'onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema ndani ya Jamii unagusa pia hata Kanisa na maisha ya kitawa. Mwaka wa Watawa si kipindi cha kuomboleza kana kwamba, watawa wamefungiwa kwenye chumba cha maiti!

Bali hiki ni kipindi cha mageuzi na matumaini si katika nguvu na uwezo wa kibinadamu, bali kwa Kristo mwenywe anayeongoza mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa. Ni matumaini kwamba, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zilizopo, maisha ya kitawa ndani ya Kanisa yataendelea kuwapo na hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuwapokonya watawa matumaini waliyo nayo!

Kardinali Joao Braz de Aviz anasema, watawa wanatambua kwamba, wanaishi kwa ari na matumaini yanayopaswa kuimarisha: upendo, urafiki na umoja. Haya ni maisha ya watawa wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili. Kumbe, lengo la tatu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni kipindi cha Kuinjilisha wito wa kila mtawa na kushuhudia uzuri na furaha ya kuwa mfuasi wa Kristo katika hali mbali mbali zinazojieleza katika maisha ya kitawa. Mwaliko wa kuchuchumilia urithi wa utajiri mkubwa walioachaiwa na waanzilishi wa Mashirika yao.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watawa kuwaamsha walimwengu kwa njia ya ushuhuda wao wa kinabii, kwa kuonesha mshikamano wa dhati kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni mwaliko wa kuendelea kuandika historia yenye mvuto na mashiko kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kamwe watawa wasijiridhishe na historia kubwa iliyoandikwa na Mashirika yao kwa miaka iliyopita! Watawa waendelee kufanya mabadiliko na mageuzi ya ndani mintarafu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. waoneshe ujasiri, uaminifu na ugunduzi.Kimsingi anasema, Kardinali Joao Braz de Aviz haya ndiyo malengo makuu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, hapo Mwaka 2015.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, wangependa kumshauri Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mwaka wa Watawa Duniani uzinduliwe rasmi mwezi Oktoba, 2014 na kufungwa Mwezi Novemba 2015. Tarehe rasmi ya kuzindua Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani inatarajiwa kuwa ni tarehe 21 Novemba 2014, Siku ya Watawa wa Ndani Duniani. Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mkutano wake unaotarajiwa kufanyika hapo Mwezi Novemba utajadili kwa kina na mapana changamoto za maisha ya kitawa mintarafu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kutafanyika makongamano na semina za kimataifa mjini Roma kwa kuwashirikisha watawa walioweka nadhiri zao katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Mkutano wa walezi; kongamano la maisha ya kitawa; ushirikiano na vyuo vikuu vya kipapa na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ili kuangalia changamoto na matumaini ya maisha ya kitawa kwa siku za usoni. Onesho la maisha na karama za kitawa kimataifa pamoja na kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yanatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 21 Novemba 2015 sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Hati ya Mapendo Kamili, yaani Perfectae Caritatis, ilipochapishwa. Baraza la Kipapa litachapisha barua ya wazi kila baada ya miezi mitatu, ili kujadili kwa kina na mapana baadhi ya mambo yanayogusa maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa. Mkazo mkubwa katika Maadhimisho haya ni malezi na majiundo makini ya watawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linaendelea kuandaa Nyaraka kuhusu: Mapitio ya uhusiano kati ya Maaskofu na Watawa; Uhuru wa Mashirika ya Kimonaki: Maisha na Utume wa Mabruda ndani ya Kanisa pamoja na hati kuhusu Mali na urithi wa watawa. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, linaendelea kupokea ushauri kutoka kwa wakuu wa Mashirika ili kuhakikisha kwamba, Mwaka wa Watawa Duniani unaadhimishwa kikamilifu mintarafu Malengo yaliyowekwa na Mama Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.