2014-01-31 10:55:56

Wanachama wa Ukatekumeni Mpya kukutana na Papa Francisko mjini Vatican tarehe 1 Februari 2014! Vatican hapatoshi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe Mosi Februari 2014 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wanachama wa Jumuiya ya Ukatekumeni Mpya, kama sehemu ya maadhimisho ya arobaini ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa mataifa.

Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya hii watatumwa kwenda kutangaza Injili ya Furaha barani Ulaya, Amerika na Australia. Jumla ya wanachama 1500 watapata baraka na hatimaye kutumwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha. Baba Mtakatifu amekwisha wahi kukutana na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Ukatekumeni mpya, lakini Jumamosi, itakuwa ni mara ya kwanza kukutana na Wanajumuiya hawa wanaoanza hija ya maisha yao ndani ya Chama hiki cha kitume.

Wale watakaotumwa watapewa Msalaba wa Kimissionari na Baba Mtakatifu Francisko ili kwenda kutangaza hekima ya Mungu inayofumbatwa juu ya Msalaba. zaidi ya watu elfu kumi wanatarajiwa kuhudhuria katika mkutano huu na Baba Mtakatifu Francisko.

Chama hiki kinapenda kuendeleza changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaowahamasisha Wakristo kugundua tena ndani mwao ile furaha ya Ubatizo kwa kuitolea ushuhuda pamoja na kuwamegea pia jirani zao!







All the contents on this site are copyrighted ©.