2014-01-31 14:11:38

Shirikianeni na Maaskofu Mahalia na Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa ili kulinda na kutunza hazina ya imani ya Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 31 Januari 2014 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa waliohitimisha mkutano wao wa Mwaka hapa mjini Vatican. Baraza hili lina uhusiano wa pekee na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani wa kuwaimarisha ndugu zake katika imani sanjari na kuendelea kulinda na kutetea Mafundisho ya Mama Kanisa.

Wajumbe wa Baraza hili wanapaswa kuhakikisha kwamba vigezo vya imani vinapewa kipaumbele cha kwanza katika maneno na matendo ili kuendeleza uwepo wa Mungu unaozaa matunda! Imani kwa Yesu Kristo inaufungua moyo wa Mungu na maisha ya mwanadamu ili kuweza kuuona ukweli na mazuri yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mafundisho tanzu ya Kanisa si sera wala siasa, ni mambo msingi yanayopania kuwasaidia Watu wa Mungu ili kuwa na msingi imara wa imani, bila kumiliki zawadi ya ukombozi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwamba, wamekabidhiwa dhamana nyeti, inayowahamasisha kushirikiana kwa karibu zaidi na Maaskofu mahalia na Tume za Mafundisho tanzu ya Kanisa katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Ili kulinda na kudumisha hazina ya imani ya watu wa Mungu katika usafi na utimilifu wake.

Wajumbe wanapaswa kujenga majadiliano endelevu na yenye kuheshimiana na wahusika. Ukweli hauna budi kujikita katika uaminifu na upendo, ili kujenga na kuimarisha udugu na ukomavu katika mawazo ya mtu! Baraza hili linajipambanua kwa kujikita katika umoja na majadiliano, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni mahali pa kujenga umoja kila mtu akijaribu kutekeleza wajibu wake aliokabidhiwa na Kristo.

Utume huu, uwajengee ndani mwao ari ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Watambue kwamba kwa neema wamebahatika kuwa ni wafuasi wa Kristo wanaoshiriki katika utume wa Kanisa katika azma ya Uinjilishaji, jambo linalowakirimia furaha ya kweli.

Wajumbe wamejadili pamoja na mambo mengine kuhusu Imani na uhusiano wake katika Sakramenti ya Ndoa, changamoto iliyokuwa imetolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipokutana nao kwa mara ya mwisho. Kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu uhusiano uliopo kati ya imani ya mtu binafsi na Maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa, mintarafu utamaduni mambo leo.

Amewapongeza kwa kazi kubwa waliyoijadili kuhusiana na changamoto katika maisha ya ndoa na falimia, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na kwamba, watoto wadogo wanapaswa kulindwa katika mazingira ya Kanisa ili waweze kukua na kukomaa kiutu na kiroho!

Baba Mtakatifu anasema anapenda kuunganisha Tume ya Kipapa ya kulinda na kutetea watoto katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa wadau mbali mbali wanaotaka kulinda na kutetea mafao ya watoto.









All the contents on this site are copyrighted ©.