2014-01-31 14:43:15

Pinda azindua rasmi mapitio ya mfumo wa uwekezaji Tanzania


Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika katika masuala ya uwekezaji nchini endapo itatekeleza kikamilifu Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji yaliyowasilishwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD). Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Januari 31, 2014, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kitabu cha Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa malengo ya mapitio ya mfumo huo ni kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini ambayo matokeo yake yatasaidia kuongeza wawekezaji katika maeneo mengi. “Kuna maeneo ya uwekezaji yanayopata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (Foreign Direct Investment -FDI) ambayo ni umeme, mafuta, gesi, madini, viwanda, ujenzi na huduma za jamii.”

Amesema kuwa matokeo ya jitihada hizi ni makubwa na yameonekana ndani ya miaka miwili tu. Akitoa mfano, alisema: “Kilimo kimeweza kukua kutoka dola za marekani milioni 304.5 mwaka 2010 hadi dola za marekani milioni 355.4 katika mwaka 2011. Vilevile kwenye sekta ya Umeme na Gesi imekua kutoka dola za kimarekani milioni 328.6 hadi dola za kimarekani 539.8 mwaka 2011.”

Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi zikiwemo rasilimali, nafasi yake kijiografia na historia ya siasa safi ambazo zinaifanya iwe kivutio kikubwa cha uwekezaji. Hali hiyo Waziri Mkuu alisema, imesaidia Pato la Taifa kuendelea kukua kwa asilimia sita kwa miaka 10 mfululizo na mwaka jana ilikua kwa asilimia saba na sasa inatarajiwa kufika asilimia 7.2 kwa mwaka huu.

Miongoni mwa maeneo yanayohusishwa na mfumo huu wa mapitio ya Uwekezaji ni yale yaliyoainishwa katika Matokeo makubwa sasa ambayo ni Kilimo, Maji, Uchukuzi, Elimu na Nishati. “Ili kufanikisha maeneo hayo ni muhimu tukajenga mazingira bora ya uwekezaji, hivyo Serikali inawataka wadau wote kwa kushirikiana na Sekta binafsi kuchambua kwa makini mapendekezo ya mapitio ya mfumo huo ambayo yanatumika pia kuharakisha mafanikio ya Matokeo makubwa sasa”, alisisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania inashukuru sana Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) kwa kuweka sura maalum kwenye kitabu hicho inayozungumzia changamoto za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Ninatumaini kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya utaongeza ufanisi wa mchakato huu na kuhakikisha kuwa tunazitumia fursa zilizopo na nyingine zaidi katika kuboresha uwekezaji katika kilimo nchini. Na kwenye kilimo ninamaanisha kilimo mazao, mifugo, uvuvi na nyuki,” aliongeza.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya OECD, Bw. Rintaro Tamaki, alisema mazingira ya uwekezaji nchini yanabadilika kila mara kutokana na kuvumbuliwa kwa rasilimali mpya kama vile gesi, makaa ya mawe ambazo zinasababisha watu wavutive kuwekeza nchini. ”Kutokana na kugunduliwa na sekta hizo, Serikali isizipuuzie sekta za zamani hususan Sekta ya kilimo, cha msingi ni kuboresha sekta hii kwa kuanzisha viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yenu”.









All the contents on this site are copyrighted ©.