2014-01-31 12:24:07

Dhambi ipo! Ukicheza Shetani atakupiga ngwara!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Ijumaa tarehe 31 Januari 2014 wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewataka waamini kutambua kwamba, kuna vishawishi na wanaweza kutumbukia katika vishawishi hivi wasiposimama kidete kumpinga shetani na mambo yake.

Mfalme Daudi aliyesifika kwa ushujaa wake, lakini alipigwa kikumbo kwa tamaa ya mwanamke wa Huria na kuzaa naye mtoto! Mfalme Daudi hakuona kwamba, hii ilikuwa ni dhambi na matokeo yake, Ufalme wa Mungu ulianza kulega lega, kwani hakutambua dhambi yake na kuwa na ujasiri wa kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kutambua udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kuomba msamaha na huruma ya Mungu, ili Ufalme wa Mungu uweze kuwafikia na kuishi ndani mwao! Utukufu wa Mungu upewe kipaumbele cha kwanza kuliko majivuno ya kibinadamu, kwani neema na wokovu wa Mungu ni mambo yanayopaswa kupaliliwa kila siku!

Uzinzi ni kati ya dhambi zinazomnyanyasa mwanadamu na kumtumbukiza katika majanga mbali mbali ya maisha, kiasi cha kuendelea kusababisha ukosefu wa haki msingi za binadamu. Watu wengi wamepoteza dhana ya dhambi, hali ambayo inadharirisha Ufalme wa Mungu, kumbe kuna haja ya waamini kutambua kwamba, kuna dhambi na ina madhara yake katika maisha ya watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.