Vyuo vikuu vinahamsishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 30 Januari 2014 amekutana na kuzungumza
na Wajumbe wa Chuo Kikuu cha Notre Dame, chenye makao yake makuu huko Indiana, Marekani;
chuo ambacho kilianzishwa kunako mwaka 1842 na Padre Edward Sorin, kutoka Shirika
la Santa Croce.
Chuo hiki kwa sasa kimeamua kufungua tawi lake mjini Roma,
ili kuendeleza mchakato wa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya utajiri unaofumbatwa
katika historia, tamaduni na maisha ya kiroho. Roma ni mji ambamo watakatifu Petro
na Paulo waliyamimina maisha yao, kielelezo cha imani inayoendelea kuungamwa na mashahidi
wa nyakati zote pamoja na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya:
familia, shule na parokia.
Baba Mtakatifu amekipongeza Chuo Kikuu cha Notre
Dame kutokana na mchango wake katika elimu ya maisha ya kiroho kwa vijana wa kizazi
kipya pamoja na kutoa fursa za masomo ili wanafunzi waweze kunoa akili kwa kuweka
uwiano sawia kati ya imani na uwezo wa mtu kufikiri na kutenda, katika mchakato wa
kutafuta ukweli. Vyuo vikuu vina mchango mkubwa katika utume wa Uinjilishaji Mpya
na kwamba, Chuo Kikuu cha Notre Dame, kimechangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho
ya elimu ya msingi nchini Marekani
Utambulisho, dhamana. mchango na huduma
ya Chuo Kikuu cha Notre Dame imeendelea kubaki bila mabadiliko makubwa hata katika
Karne ya 21. Baba Mtakatifu anasema Kanisa halina budi kuendelea kukazia utambulisho
wake wa kimissionari kwa njia ya ushuhuda unaotolewa na wafuasi wa Kristo wanatekeleza
majukumu yao hata katika taasisi zinaendeshwa na kusimamiwa na Mama Kanisa; utume
huu kwa namna ya pekee, ujioneshe kwa Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya Juu, ili kuweka
sawia imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda; mambo yanayomwezesha mwanadamu
kuishi katika ukamilifu wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushuhuda wa
vyuo vikuu ni jambo la muhimu sana katika utekelezaji wa mafundisho ya maadili yanayotolewa
na Mama Kanisa; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru sanjari na kuendeleza
Mafundisho ya Kanisa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Ni matumaini
ya Baba Mtakatifu kwamba, Chuo Kikuu cha Notre Dame, kitaendelea kutolea ushuhuda
wa tunu hizi msingi katika maisha na utume wake, kwa kulinda utambulisho wa Kikristo.
Baba
Mtakatifu amewaomba wajumbe kumwombea katika maisha na utume wake kwa ajili ya Injili
ya Kristo na kwamba, anawakumbuka kwa sala na sadaka yake. Mwishoni, amewapatia baraka
zake za kitume!