Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Siku ya Jumatano, tarehe 29 Januari
2014 alikemea vikali tabia ya michezo ya upatu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu
na kwa kusema kwamba, huu si Ukristo wala si ubinadamu; ni tabia ambayo inapaswa kukomeshwa
ndani ya Jamii kwani inawasababishia watu majanga ya maisha!
Baba Mtakatifu
ameyasema hayo wakati alipokuwa anawasalimia wawakilishi wa kitaifa wa Mfuko wa Yohane
Paulo II dhidi ya upatu kitaifa, ambao baadaye jioni waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali Angelo
Comastri, Askofu msaidizi wa mji wa Vatican.
Katika mahubiri yake Kardinali
Comastri anasema mwelekeo wa watu kupenda na kuthamini mno fedha na mali, umewatumbukiza
watu wengi katika majanga ya maisha. Baadhi yao wamejikuta wakikabiliana na mkondo
wa sheria kwa kuikiuka sheria, kanuni na maadili jamii. Watu wanaabudu sana fedha
kiasi cha kuifanya kupoteza ile thamani yake kwa kunyanyasa na kudhalilisha utu na
heshima ya binadamu. Baadhi ya watu wanaifanya fedha kuwa eti sabuni ya roho na mtawala
wa maisha ya baadhi ya watu, hata utu na heshima ya mtu inapimwa kwa viti alivyonavyo
mtu na wala si utu wake kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Tamaa
ya utajiri wa haraka haraka umewatumbukiza watu katika michezo michafu ya upatu na
kamari, mambo yanayochafua utu na heshima ya binadamu. Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa
na kushuhudiwa na Mama Kanisa ni kwamba, mtu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza;
jambo msingi linalojidhihirisha katika Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani; muhtasari
wa mafundisho makuu ya Yesu yanayopaswa kumwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma.
Kardinali Comastri anasema, watu wanapaswa kujenga utamaduni wa upendo na
mshikamano na wala si kunyanyasana na kufedheheshana. Watu wasisahau kwamba, mara
baada ya kifo, mali na utajiri wa dunia hii wataiacha hapa duniani na watasindikizwa
na sanda ya matendo mema waliyowatendea jirani zao. Mshikamano wa upendo na kidugu
ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya mafundisho
na ushuhuda wa maisha yake.
Anawakumbusha watu wasitawaliwe mno na fedha na
mali, bali mambo haya yawe ni kikolezo cha mshikamano wa upendo na udugu kwa kuwajali
na kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao kwa hali na mali! Kanisa linawapongeza
mashujaa wanaosimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wanyongwe wanaoendelea
kudidimizwa na watu wenye uchu na tamaa ya mali na fedha kwa njia ya mkato.
Watu
wasikubali na kujidekeza hatimaye wakajikuta wanatumbukizwa kwenye mchezo wa upatu
na kamari kwani ni hatari kwa maisha na maendeleo yao! Anasema Kardinali Angelo Comastri
wakati anahitimisha mahubiri yake!