Fadhila ya unyenyekevu, uaminifu na maisha ya sala ni muhimu sana kwa utambulisho
wa Mkristo ndani ya Kanisa!
Ni dhana isiyoweza kueleweka kwa mtu kujiita Mkristo pasi ya kuwa sehemu ya Kanisa!
Unyenyekevu, uaminifu na maisha ya sala ni mambo muhimu sana yanayoweza kumtambulisha
mwamini kuwa kweli ni Mkristo.
Mfalme Daudi alitambua kwamba, alikuwa ni sehemu
ya Taifa la Mungu, anafurahia kuzungumza na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala na kupokea
changamoto zinazowekwa mbele yake, changamoto kwa waamini kujisikia kuwa ni sehemu
ya Kanisa na ndani ya Kanisa.
Haitoshi kwa mwamini kupokea Sakramenti ya Ubatizo
na baadaye kutokkomea "mitini" akaendelea kujiita kuwa ni Mkristo; kwa kudhani kwamba,
anamsikiliza Kristo lakini kwa upande mwingine analibeza na kulitweza Kanisa lililoanzishwa
na Kristo mwenyewe! Huwezi kuwa Mkristo wa kweli kwa kusimama pembezoni mwa Kanisa,
Kanisa linajengwa na kuimarishwa kwa njia ya utakatifu na mshikamano unaowawezesha
waamini kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Kama fadhila ya unyenyekevu inapwelea katika maisha ya mwamini hapa kuna shida,
kwani mtu atashindwa pia kuutambua ukuu na utukufu wa Mungu kama alivyofanya Mfalme
Daudi kama anavyosimuliwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, Alhamisi, tarehe 30 Januari
2014.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye
Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Anasema, historia ya ukombozi
ni mchakato ulioanzishwa na Mwenyezi Mungu na kuendelezwa na Mama Kanisa kwa watu
wa nyakati mbali mbali. Unyenyekevu uwasaidie watu kutambua kwamba, wao ni sehemu
ya Familia kubwa ya Mungu ulimwenguni.
Unyenyekevu, uaminifu na utii ni fadhila
muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanapaswa kuwa waaminifu kwa
Kristo na Kanisa lake; waaminifu kwa Kanuni ya Imani na Mafundisho ya Kanisa, kwa
kutambua kwamba, wamebarikiwa kupata Injili ya Kristo kama zawadi, changamoto na mwaliko
wa kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha wengine zawadi hii kwa uaminifu mkubwa.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuliombea Kanisa
katika maisha na utume wake! Utume huu upate chimbuko lake kuanzia kwenye familia
ili waamini waendelee kutambua na kuthamini hija hii inayowasaidia kujisikia kuwa
wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.