Changamoto katika maisha ya kitawa na Kipadre! 2015 ni Mwaka wa Watawa
Uaminifu na udumifu wa wito wa kitawa katika tamaduni za mpito ni mada ambayo imepembuliwa
kwa kina na mapana hivi karibuni kwenye Kongamano la siku moja lililoandaliwa na Chuo
Kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko mjini Roma na kuwashirikisha viongozi wakuu
kutoka Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.
Askofu mkuu
Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na
Kazi za Kitume akichangia mada kwenye Kongamano hili anabainisha kwamba, hali ya miito
kwa Mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume ni tete!
Mashirika haya yanahamasishwa
zaidi na zaidi kujikita katika malezi msingi na endelevu kwa ajili ya watawa ili kuweza
kuimarisha hali ya miito inayoendelea kulega lega siku hadi siku na hivyo kusababisha
watawa wengi kutoona tena thamani ya maisha na wito wao wa kitawa na hivyo kuamua
kuachia ngazi! Inasikitisha kuona kwamba, hata wale ambao wameishi kwa miaka mingi
katika utawa wanaanza kukata tamaa na kuondoka.
Idadi kubwa ya watawa wa kiume
na kike wanaoacha utawa ni dalili za mtikisiko wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa.
Haya ni matokeo ya myumbo wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; imani, maadili
na utu wema. Haya ni matokeo ya utandawazi yanayojionesha hata ndani ya Kanisa, kwa
sababu watawa ni watu waliochaguliwa kutoka katika Jamii kwa ajili ya mambo ya Kimungu,
lakini bado wanaendelea kubakia na ubinadamu wao uliojeruhiwa kwa dhambi ya asili.
Kimsingi anasema Askofu mkuu Carballo hizi ni athari za myumbo wa: uchumi, kijamii,
kitamaduni na kimaadili.
Anasema, si rahisi kutambua kwa haraka haraka idadi
ya watawa wanaoachia ngazi ya wito na maisha ya kitawa, kwani kuna Mabaraza mawili
ya Kipapa yanayoshughulikia kesi za namna hii. Kwa watawa, kesi hii inashughulikiwa
na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na kwa upande wa Watawa
Makleri, kesi zao zinashughulikiwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri na kesi
zenye utata wa imani na maadili zinashughulikiwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho
Tanzu ya Kanisa.
Katika kipindi cha Miaka mitano iliyopita, yaani kuanzia Mwaka
2008 hadi mwaka 2012, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, limetoa
ruhusa kwa watawa 11, 805 kuacha rasmi wito na maisha ya kitawa. Huu ni wastani wa
watawa 2, 361 wanaoacha maisha ya kitawa kwa Mwaka.
Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Makleri katika kipindi cha Miaka mitano iliyopita, limetoa kibali cha kuwasimamisha
Mapadre 1, 188 na Mashemasi 130. Kwa pamoja idadi hii ya Watawa na Mapadre walioacha
ni 13, 123. Hali hii inatisha na kusikitisha sana. Wote hawa ni wastani wa Watawa
na Mapadre 3,000 wanaoacha wito na maisha yao kitawa na kipadre kwa mwaka. Pengine
kuna mambo mengi ambayo yamefichika chini ya idadi hii na kwamba, kuna haja kwa Kanisa
kuliangalia tatizo hili kwa jicho la pekee ili kuweza kuimarisha miito ya kitawa na
kipadre kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni.
Askofu
mkuu Carballo anasema kuna baadhi ya mambo yanayochangia kasi kubwa ya watawa na mapadre
kuacha wito na maisha yao. Jambo kubwa na sababu msingi ni ukavu wa maisha ya kiroho.
Watawa na Mapadre wanajikuta hawana tena hamu yak usali, kutafakari wala kushiriki
Sakramenti za Kanisa zinazowakirimia neema na baraka katika maisha na wito wao.
Sala
za binafsi na zile za Kijumuiya hazina nafasi tane, pengine kwa kisingizio cha kuelemewa
mno na kazi za kitume! Hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya
kiroho na kiimani na matokeo yake kuitema zawadi ya utawa na upadre, waliyoipokea
kwa shangwe na nderemo wakati walipokuwa wanaweka nadhiri au kupadrishwa.
Katika
hija ya maisha ya kitawa na kipadre, baadhi yao hupoteza utambulisho wao kwa Jumuiya,
Shirika na hata wakati mwingine kwa Kanisa lenyewe. Dalili zake ni watu kutoridhika
na maisha ya Kijumuiya, kinzani, migogoro na hali ya kudhaniana vibaya. Ubaguzi na
upendeleo unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Mashirika na Jumuiya za Kitawa, ni mambo
yanayochangia kuwafanya baadhi ya watawa na mapadre kutoshiriki kikamilifu katika
maisha ya Kijumuiya kwa kutindikiwa uwiano makini kati ya maisha ya mtu binafsi na
yale ya Kijumuiya au Kishirika. Matokeo yake, watu hawa watatafuta fursa hizi nje
ya Jumuiya na Mashirika yao, mwanzo wa kuchanganyikiwa na kuanza pole pole kupoteza
dira na mwelekeo wa maisha ya kitawa na kipadre.
Kumbu kumbu zinaonesha kwamba,
uhusiano kati ya mtawa na mtawa, au kati ya mtawa na viongozi wake ni chanzo cha watawa
na mapadre wengi kuachia ngazi. Hii ni kutokana na hali ya kutoelewana, ukosefu wa
majadiliano ya kina yanayosimikwa katika msingi wa ukweli na uwazi; upendo na huruma.
Majadiliano ya kina yanapogeuka kuwa ni majanga ya Kijumuiya, hapo kuna hatari ya
watawa kuacha utawa.
Baadhi ya watawa na mapadre hawakubaliani kimsingi na
Mafundisho tanzu ya Kanisa, hali inayoonesha mpasuko wa kiimani na kimaadili katika
utekelezaji wa wito na maisha ya kitawa na kipadre. Wengine wanashindwa kutatua kinzani
hizi kwa njia halali na matokeo yake wanakosa mwelekeo. Baadhi ya mafundisho ambayo
yanasadikiwa kuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kitawa na kipadre ni suala
la useja na hata wakati mwingine, kumongo’onyoka kwa maadili katika fadhila hizi na
hivyo kuwafanya baadhi ya watawa na mapadre kuwa na mwelekeo potofu hata wakati mwingine
kusababisha kashfa.
Hawa ni watu ambao mioyo yao imegawanyika na mara wanapoacha
wanaona hakuna kitu cha thamani ambacho wamekipoteza, kwani: utawa au upadre ilikuwa
ni sawa na Hoteli au nyumba ya mapumziko
Askofu mkuu Carballo anasema, pengina
kuna haja ya kuangalia kwa makini historia, maisha na mahali wanapotoka vijana wanaoomba
kujiunga na maisha ya kitawa na kipadre. Jumuiya zinazowapokea na kuwaanzishia mchakato
wa malezi na majiundo yao msingi zinapaswa kuwa makini kwa kusoma alama za nyakati
kwani sasa mambo mengi yamebadilika kutokana na athari za utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Kuna mabadilio ya vipaumbele katika maisha; kuna vielelezo
vipya vya maisha na tunu msingi; mambo ambayo yanasambazwa kwa kasi ya ajabu na hata
pengine kusababisha mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili.
Mwingiliano wa
tamaduni na kinzani hizi unawachanganya watu kiasi cha kushindwa wakati mwingine kutambua
mambo msingi katika maisha na wito wa kitawa na kipadre! Thamani na utu wa mtu unapimwa
kwa mchango wake katika Jumuiya! Wanathaminiwa wale wanaochangia kwa kiasi kikubwa
na wengine wanaambulia patupu! Watu wanaelemewa na utamaduni wa mpito, hawataki kufungwa
na maisha ya kitawa na kipadre, wanataka kwenda nje, kula kuku kwa mrija! Lakini wanapofika
huko, baada ya muda si mrefu wanatambua kwamba, wamejichumia “majanga” ya maisha!
Ubinafsi
unatawala zaidi kuliko maisha ya Kijumuiya na kwamba, watu wanataka uhuru usiokuwa
na mipaka, kinyume cha Mashauri ya Kiinjili. Njia za mawasiliano ya jamii na mawasiliano
kwa ujumla yameboreshwa, lakini bado watu wengi wanashindwa kukutana na jirani zao,
wanabaki wamejifungia katika ubinafsi wao!
Askofu mkuu Carballo anasema, licha
ya hali hii inayoonesha mtikisiko wa maisha na wito wa kitawa na kipadre, lakini bado
kuna idadi kubwa ya watawa na mapadre wanaoishi na kufurahia wito wao kwa ajili ya
Mungu na jirani katika sekta mbali mbali za maisha: katika katekesi, elimu, afya na
maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: Ni watu wanaorutubisha maisha yao ya kiroho
kwa Ibada, Sakramenti, Neno la Mungu na matendo ya huruma. Hawa ndio wale wanaomtafuta
na kutaka kuishi karibu na Mwenyezi Mungu, wakimpatia kipaumbele cha kwanza katika
maisha na utume wao, tayari kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa kinabii ambao wakati
mwingine unasigana na malimwengu.
Kanisa linahitaji watawa na mapadre wema
na watakatifu; bila kusahau kwamba, hata katika kundi hili bado wadhambi wataendelea
kuwamo, jambo la msingi ni kujitambua na kuanza hija ya toba na wongofu wa ndani,
inawezekana kufurahia wito na maisha kitawa na kipadre, kila mtu akitekeleza wajibu
na dhamana yake barabara!
Kanisa liendelee kuwekeza katika majiundo msingi
na endelevu, daima likijitahidi kusoma alama za nyakati. Watawa na Mapadre katika
miaka yao ya kwanza kwanza, wasaidiwe kikamilifu kuwa na dira na mwongozo wa maisha,
wasije wakamezwa na malimwengu.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.