Wadau wa mawasiliano ya kijamii wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kuwajibika!
Mabingwa na wadau katika sekta ya mawasiliano ya Jamii baada ya warsha ya siku moja
iliyofanyika mjini Roma, wamekubaliana kimsingi na changamoto iliyotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko kwamba, kuna haja ya kujenga mawasiliano katika msingi wa maadili
na uwajibikaji, kwa kutambua kwamba, mawasiliano yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma
na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana.
Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais
wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika mkutano huu, amewasilisha muhtasari
wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni,
itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe Mosi, Juni, 2014 sanjari na Siku kuu
ya Kupaa Bwana Mbinguni. Neno msingi ni ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu.
Warsha
hii iliandaliwa na Mfuko wa Uinjilishaji kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii,
kwa kuongoza na kauli mbiu "mawasiliano yajayo yanasimikwa katika uwajibikaji". Askofu
mkuu Celli anasema, tatizo kubwa linaloikabili sekta ya mawasiliano ya jamii si teknolojia
bali ni mtu anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kujenga na kudumisha mahusiano
kati ya watu. Hii ni changamoto inayoligusa Kanisa katika maisha na utume wake sehemu
mbali mbali za dunia kwa kujikita zaidi katika ushuhuda wa imani tendaji.
Mabingwa
na wadau hawa wanasema watu wamechoka kusikia mafuriko ya maneno, wataka sasa kushuhudia
imani katika matendo! Maadili ni jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele katika
sekta ya mawasiliano ya Jamii! Wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano wanapaswa kuwa
waaminifu kwa kazi yao, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu.
Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kupeta katika mchakato wa mawasiliano ya kijamii kiasi cha kumpiku
hata Rais Barack Obama wa Marekani. Watu wanavutwa zaidi na Papa Francisko kwa maneno
yake yanayogusa sakafu ya mioyo ya wengi, vitendo vyake vinaonesha kujali na kuthamini
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Wadau wa habari wajenge
na kuzingatia maadili kwani vyombo vya mawasiliano ya Jamii kwani vina umati mkubwa
wa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kwa shughuli mbali mbali. Wawe makini kutunza
na kudumisha tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu.