2014-01-29 12:00:20

Roho Mtakatifu anawakirimia waamini neema ya kushikamana na maskini kwa kushuhudia Injili ya Furaha na Amani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 29 Januari 2014 aliendelea kutoa Katekesi kuhusu Sakramenti Saba za Kanisa, kwa kukazia Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo, yaani Ubatizo, Ekaristi Takatifu na Kipaimara ambazo huweka misingi ya maisha yote ya Kikristo.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ametafakari juu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa kusema kwamba, Sakramenti zinawawezesha waamini kushiriki katika Fumbo la Kifo na Ufufuko wa Kristo na hivyo kuwa ni viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Katika Sakramenti ya Kipaimara, waamini wanapokea mhuri wa Roho Mtakatifu kwa kupakwa mafuta ya Krisma ya Wokovu, ili kufanana zaidi na Kristo, Mpakwa wa Mungu. Waamini wanaimarishwa katika neema ya Sakramenti ya Ubatizo na katika utume wao, tayari kumtolea Kristo na upendo wake, ushuhuda wa maisha. Kazi ya Roho Mtakatifu inajidhihirisha katika maisha ya waamini kwa njia ya karama za Roho ambazo ni: hekima na akili; ushauri na nguvu; elimu, ibada na uchaji wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwakirimia neema kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, iliyowajaza furaha ya Roho Mtakatifu, ili daima waendelee kuwa ni kioo cha Kristo katika ujenzi wa mahusiano na wengine; kwa kuwa wazi kwa wahitaji sanjari na kushuhudia Injili ya Furaha na Amani.

Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba, kwa kuimarishwa kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wanachangamotishwa na Mama Kanisa kumshuhudia Kristo na Kanisa lake bila ya kuogopa! Wajitahidi kumfungulia Kristo milango ya mioyo ya maisha yao, ili aweze kutenda kazi kati yao kwa: kusali, kusamehe, kuwaonjesha wengine matumaini na faraja; kwa kuhudumia na kushikamana pamoja na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; tayari kujenga na kuimarisha umoja sanjari na kupandikiza mbegu ya amani kati ya watu.

Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote katika ujumla wao kuwa ni Wasamaria wema kwa maskini na wakimbizi. Serikali na wadau mbali mbali waendelee kushirikiana ili kutengeneza fursa za ajira kwani kazi ni kiini cha utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.