Makumbusho ya Vatican ni kati ya vivutio vikuu mjini Vatican, ukibahatika kufika huko
nenda kashangae maajabu ya Mungu!
Zaidi ya watu millioni 5. 5 walitembelea Makumbusho ya Vatican katika kipindi cha
Mwaka 2013. Hii ni habari njema kwa kuona kwamba, kuna mamillioni ya watu wanaovutwa
kutembelea hazina kubwa ya binadamu inayohifadhiwa kwenye Makumbusho ya Vatican.
Watu zaidi ya millioni mbili kila mwaka hutembelea kitengo cha “Uffizi”.
Mkurugenzi
mkuu wa Makumbusho ya Vatican, Bwana Antonio Paolucci anasema kwamba, idadi hii ni
kubwa mno kuweza kuhudumiwa kwa ufanisi mkubwa na kwamba, wakati mwingine kuna hatari
ya kuweza kuharibu kumbu kumbu hizi kutokana na wingi wa watu pamoja na msongo wa
mawazo kwa wahudumu, wanaopania daima kutoa huduma iliyotukuka kwa ufasaha na tija.
Pamoja
na changamoto hizi, Makumbusho ya Vatican yanayotembelewa na watu wengi kutoka: Japan,
Canada, Chile, Brazil, Australia yataendelea kutoa huduma yake na wala hayana mpango
wa kuweka idadi maalum, kwani wengine huwa ni mara yao ya kwanza kushuhudia utajiri
huu wanapopata nafasi ya kutembelea mjini Vatican. Wengi wanapenda kushuhudia umahiri
wa Sanaa ulioneshwa kwa namna ya pekee kwenye Kikanisa Cha Sistine na kwenye Chumba
cha Raphael; Laocòòn na eneo la Apollo Belvedere.
Bwana Antonio Paolucci anasema,
uongozi wa Vatican unadhibiti idadi ya watu wanaotembelea Makumbusho ya Vatican kwa
kuhakikisha kwamba, kuna mgawanyo mzuri wa watu kwa siku nzima bila ya mwingiliano
mkubwa, ili kuwapatia watalii nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani
kwa matendo makubwa aliyomwezesha mwanadamu kuyatenda kwa hekima na busara.
Uongozi
unawashauri watalii wanaotaka kutembelea Makumbusho ya Vatican kuhakikisha kwamba,
wanafanya mipango yao kwa njia ya mtandao, ili kuokoa rasilimali muda. Mpango huu
unaonekana kupata ufanisi mkubwa, kiasi kwamba, Makumbusho ya Vatican yaliweza kupokea
watalii zaidi ya millioni 5. 5 katika Kipindi cha Mwaka 2013.
Makumbusho ya
Vatican kadiri ya bajeti yake, yataendelea kuboresha Sanaa zilizopo, ili kuleta mvuto
zaidi na hatimaye kuzima kiu ya watalii wanaotaka kutembelea utajiri wa Makumbusho
ya Vatican. Mkakati huu unakwenda sanjari na ukarabati pamoja na uimarishaji wa hifadhi
ya Sanaa zilizopo, kwani penye wengi kuna mengi! Uongozi unajipanga barabara ili kuwa
na mapokezi mazuri kwa watalii pamoja na kukabiliana na changamoto mpito kwa kuwapangia
vyema watalii bajeti yao!